WAKALA WA MCHEZAJI KYLIAN MBAPPE AMETHIBITISHA MCHEZAJI HUYO KUJIUNGA NA REAL MADRID MAJIRA YA KIANGAZI
Wakali wa Kylian Mbappe, ambaye ni mama yake mzazi amefichua supastaa huyo wa kimataifa wa Ufaransa atajiunga na Real Madrid kwa uhamisho wa bure dirisha hili la majira ya kiangazi.
Mbappe, 25, ataachana na Paris Saint-Germain na hilo ameshalithibitisha kutokana na mkataba wake kufika tamati mwishoni mwa mwezi ujao.
Ikiwa bado haijatangazwa ni wapi atakwenda msimu ujao, ripoti zinadai Real Madrid inaonekana kuwa kwenye nafasi ya kunasa saini yake.
Los Blancos inayonolewa na Carlo Ancelotti inatarajia kutangaza dili hilo mapema mwezi ujao, wakati itakapomalizana na Borussia Dortmund kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya uwanjani Wembley.
Mbappe alifanya sherehe Jumatatu huko Paris akihitimisha muda wake wa kuwapo kwenye kikosi cha PSG na wakala wake, ambaye pia ni mama yake, alifichua ni wapi atakwenda kucheza msimu ujao.
"Wote mshafahamu tayari," alisema mrembo Fayza Lamari, alipoulizwa klabu inayofuata ya mwanaye.
Wachezaji wenzake Mbappe wanaripotiwa walikuwapo kwenye sherehe hiyo, lakini Kocha wa PSG, Luis Enrique na Rais Nasser Al Khelaifi hawakuwapo.
Mbappe alifunga mabao 44 na kuasisti mara 10 katika mechi 47 alizocheza kwenye klabu hiyo ya PSG kwa msimu huu na kufanikiwa kubeba taji la Ligue 1.
Kikosi hicho cha Enrique kitacheza na Lyon kwenye fainali ya Coupe de France wikiendi hii, lakini kinachoelezwa, huenda Mbappe akawekwa kando kwenye kikosi kwa ajili ya mechi hiyo.
Kwa jumla yake, Mbappe amefunga mabao 256 na kuasisti 108 katika mechi 307 alizocheza PSG.