KATIKA utambulisho wa wachezaji kwa ajili ya msimu wa mwaka 2024/25, klabu ya simba sc haija orodhesha jina la gwiji huyo. Wako wengine ambao hawakutambulishwa kama Willy Onana na Israel Mwenda, lakini hawana uzito huo wa Aishi Manula.

Wakati ule wa usajili wa kutotumia mikataba, ilikuwa rahisi kwa klabu kutomwambia lolote mchezaji hadi siku ya mwisho ya usajili anapojikuta hayumo kwenye orodha ya klabu aliyokuwa anaichezea na kwa jumla hayumo kwenye usajili wa klabu yoyote hadi msimu mwingine.

Wakati huo hakukuwa na dirisha la katikati ya msimu. Usajili ulikuwa mwanzoni mwa msimu pekee. Hivyo mchezaji anayeachwa dakika za mwisho hukosa timu ya kuichezea hadi msimu mwingine unapofika. Wachezaji wengi waliteswa na ukatili huu wa viongozi, ambao wakati mwingine ulilenga kumkomoa mchezaji au kutokuwa na maamuzi thabiti yanayotokana na mikakati mizuri ya kuunda timu.

Lakini adha hii haikuwagusa wale wachezaji nyota kwa kuwa viongozi waliwawekea mikakati maalumu na hivyo mwishoni mwa msimu hawasumbuki. Wachezaji hao nyota nao walikuwa na mitego yao ya kuwakosesha kucheza msimu mzima.

Baada ya kusajili timu moja, nyota hao walibembelezwa hadi kukubali kusajili timu nyingine na matokeo yake yakawa ni kusajili timu mbili, kitu ambacho kikanuni hakikuruhusiwa na adhabu ikawa ni kufungiwa kucheza msimu mzima.

Hayo ni ya kale yalipita na ustaarabu wake kwa kuwa masuala ya mikataba yaliondoa tabia za viongozi kuwatelekeza wachezaji kwa sababu yoyote ile na iwapo hali hiyo itatokea, basi mchezaji ana haki ya kwenda kwenye vyombo vya haki kudai fidia au masuala mengine.

Ustaarabu wa kufuata na kuheshimu kanuni sasa umekuwa mkubwa na klabu zinazopuuza zinakumbana na adhabu kali za vyombo vya haki vya ndani au kimataifa kama vya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) au Mahakama ya Usuluhishi wa Masuala ya Michezo (CAS).

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement