TFF YAIFUNGIA USAJILI BIASHARA UNITED
Klabu ya Ligi ya Championship ya NBC, Biashara United imefungiwa kusajili mpaka itakapomlipa aliyekuwa mchezaji wake Tayo Odongo.
Uamuzi huo umefanywa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) baada ya mchezaji huyo kushinda kesi ya madai dhidi ya klabu hiyo.
Mchezaji huyo raia wa Uganda alifungua kesi FIFA akidai malipo ya malimbikizo ya mishahara.
Klabu hiyo ilitakiwa iwe imemlipa ndani ya siku 45 tangu uamuzi huo ulipotolewa, lakini haikutekeleza hukumu hiyo.
Wakati FIFA imeifungia klabu hiyo kufanya uhamisho wa wachezaji kimataifa, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeifungia kufanya uhamisho wa ndani.
TFF inazikumbusha klabu kuheshimu mikataba ambayo zimeingia na wachezaji pamoja na makocha ili kuepuka adhabu mbalimbali ikiwemo kufungiwa kusajili.