MANCHESTER UNITED IPO MBIONI KUINASA SAINI YA STRAIKA WA KLABU YA ATLETICO MADRID ALVARO MORATA
Manchester United imeripotiwa kuwa imetuma ofa kwenda Atletico Madrid kwa ajili ya kuipata saini ya straika wa timu hiyo, Alvaro Morata katika dirisha hili.
Staa huyu wa kimataifa wa Hispania anataka kuondoka kutafuta changamoto mpya kwingineko na mbali ya Man United huduma yake inawindwa pia na Juventus, Borussia Dortmund na Fenerbahce ambazo tayari zimeshaanza mazungumzo na wakala wake.
Kwa mujibu wa tovuti ya The Mirror, katika mkataba wake na Atletico kuna kipengele kinachoiruhusu timu inayohitaji kumnunua kulipa Pauni 10 milioni.
Timu nyingi zimevutiwa naye kutokana na kiwango alichoonyesha msimu uliopita ambapo alifunga mabao 21 katika mechi 48 za michuano yote.
Mbali ya kiwango bora alichoonyesha msimu uliopita akiwa na Atletico, Morata pia ameonyesha kiwango bora katika michuano ya Mataifa ya Ulaya (Euro) akiwa na timu ya Hispania ambapo amefunga bao moja katika mechi mbili. Mkataba wake unamalizika mwaka 2026.