MAMELOADI SUNDOWNS WASAJILI KIUNGO KWA BILIONI 6.2
Wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa Simba na Yanga wakiwa wameshafunga hesabu zao katika dirisha dogo la usajili, miamba ya soka la Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns imeonyesha jeuri ya fedha kwa kutambulisha kiungo Matías Esquivel kutoka klabu ya Club Atlético Lanus ya Argentina mwenye thamani ya Sh6.2 bilioni.
Akizungumza baada ya kutambulishwa, Esquivel kupitia video fupi iliyochapishwa na klabu hiyo kwenye akaunti ya Mamelodi ya mtandao wa X(zamani Twitter) amesema; "Jina langu ni Matías Esquivel; ninajivunia kuwa wamanjano,"
Kama ilivyoripotiwa na mitandao mbalimbali huko Afrika Kusini,
Esquivel alitua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa OR Tambo mjini Johannesburg, Afrika Kusini Jumapili iliyopita.
Kuwasili kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 hakujaleta tu nguvu mpya kwenye eneo hilo bali ni mchezaji mwingine ghari zaidi kwenye kikosi hicho.
Ripoti zinaonyesha kuwa mchezaji huyo wa Argentina anayetumia mguu wa kushoto alinunuliwa na Sundowns kwa R46 milioni ambazo ni zaidi ya Sh.6.2bilioni.
"Mamelodi Sundowns imethibitisha kumsajili Matías Esquivel kutoka klabu ya Argentina ya Atlético Lanus kwa mkataba wa miaka minne na nusu,"ilisema taarifa ya klabu hiyo.
Katika usajili wa mchezaji huyo, Lanus imeweka kipengele cha kupata mgawowa asilimia 10 ikiwa Mamelodi itamuuza mchezaji huyo sehemu nyingine.
Kiungo huyo anajiunga na Masandawana ikiwa ni usajili wa pili katika dirisha hili la katikati mwamsimu, baada ya beki Zuko Mdunyelwa aliyejiunga Desemba 2023.
Kama ilivyo kwa Yanga na Simba ambapo wachezaji wake wapya wameanza kuripoti kambini kwa ajili ya maandalizi ya michezo iliyosalia kwenye mashindano ya ndani na Ligi ya Mabingwa Afrika mwamba wa Sh6.2bilioni naye tayari ameanza mazoezi.
Akiwa Amerika Kusini ambako alikuwa akiichezea Lanus, alifunga mabao sabana kutoa asisti 12 katika mechi 95.