YANGA imemaliza operesheni makombe, sasa wamerudi mezani kurekebisha kikosi. Wameanza mazungumzo rasmi na staa Mkongoni, Makabi Lilepo wa Al Hilal ya Sudan.


Makabi ambaye ni swahiba mkubwa wa Henock Inonga wa Simba, ameomba kibali cha kutafuta timu kwa muda atakayoichezea hata kwa mkopo kuokoa kiwango chake kutokana na hali ya machafuko nchini Sudan.


Mwanaspoti linajua kwamba katika majina ya klabu tatu zilizomfuata mchezaji huyo, ameielewa zaidi Yanga ambayo hata kabla hajaenda Sudan ilikuwa inamtamani.

Mwanaspoti linafahamu kuwa mshambuliaji huyo mwenye kasi yuko katika mazungumzo mazuri na Rais wa Yanga injinia Hersi Said ambaye hii ni hatua ya pili kwake kutaka huduma ya Lilepo ambaye hata Simba wanamtaka.


Mapema Hersi aliwahi kuhitaji huduma ya Lilepo kabla ya kusajiliwa na Al Hilal lakini klabu yake ya AS Vita ilihitaji kiasi kikubwa cha fedha hatua ambayo iliwafanya Yanga kunyoosha mikono.


Lilepo kitu ambacho bado anashindana na Yanga kwa sasa ni mshahara mkubwa ambao Yanga inamtaka aushushe ili aje kwa mabingwa hao kuanzia msimu ujao akakiwashe kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kuanzia Agosti 18.


Yanga inataka kuiongezea makali safu yake ya ushambuliaji kwa msimu ujao na mtu bora na chaguo lao la kwanza limebaki kwa Lilepo ambaye pia amekuwa akihitajiwa kitambo na kocha wao Nasreddine Nabi anayehusishwa na kujiunga na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.


Kitu kikubwa ambacho kimemuingia kwenye akili Lilepo ni hatua ya Yanga kucheza fainali ya kombe la shirikisho, huku pia akijua anaungana na wenzake Wakongomani akiwemo Fiston Mayele ambaye yuko naye kambini kwenye kikosi cha taifa lao la DR Congo.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement