Klabu ya Geita Gold leo Desemba 20 imetangaza kuachana na kocha wake mkuu, Hemed Suleman 'Morocco' huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni kubanwa na majukumu ya timu ya taifa Taifa Stars'.

Taifa Stars inajiandaa na michuano ya Kombe la ataifa ya Afrika (AFCON) inayotarajia kuanza Januari mwakani, nchini Ivory Coast.

Geita Gold imetoa taarifa kwa umma leo Desemba 20, 2023 ikitangaza kuachana na kocha huyo ambaye amedumu klabuni hapo kwa miezi sita tangu alipotambulishwa Julai 21, mwaka huu kuchukua mikoba ya Fredy Felix 'Minziro'.

Morocco ambaye ni kocha msaidizi wa Stars, ameiongoza Geita Gold katika michezo 12 ya Ligi Kuu akishinda mitatu, sare nne na kupoteza tano, akivuna pointi 13 na kukamata nafasi ya 13, huku kikosi chake kikifunga mabao nane na kuruhusu 14.

Pia ameisaidia timu hiyo kutinga hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) baada ya ushindi wa mabao 5-0 mbele ya Singida Cluster.

Katika taarifa hiyo, uongozi wa Geita Gold umesema; "Klabu ya soka ya Geita Gold inapenda kuutangazia umma kuwa imefikia maridhiano ya kusitisha mkataba na aliyekuwa kocha mkuu wa timu yetu kocha Hemedi Suleiman" Klabu imeridhia ombi la Morocco kusitisha mkataba kwa sababu alizozitaja ikiwa ni pamoja na kubanwa na majukumu ya timu ya Taifa.

Klabu inamshukuru kwa kipindi chote alichohudumu kama kocha mkuu wa klabu yetu kwa mafanikio makubwa na pia itaendelea kumtumia kama mshauri wa klabu katika mambo ya kiufundi," Afisa Habari wa klabu hiyo, Samwel Dida ameiambia Mwanaspoti kwamba wamefikia makubaliano ya kusitisha mkataba baada ya kuona haitakuwa vizuri timu kukosa kocha mkuu kwa kipindi cha miezi miwili ambayo Morocco atakuwa na tỉmu ya Taifa nchini Ivory Coast.

Dida amesema kwa sasa timu hiyo ambayo kesho Alhamisi itamenyana na Singida Big Stars katika Uwanja wa Nyankumbu, itakuwa chini ya makocha wasaidizi, Salehe Machupa na Choki Abeid hadi hapo kocha mpya atakapopatikana.

"Kocha (Morocco) ameomba akafanye majukumu ya timu ya taifa kwa sababu majukumu ya timu ya Taifa na klabu yanambana ambapo ataondoka kujiunga na Stars kwa ajili ya AFCON itakayocheza karibu miezi miwili; "Kwahiyo timu kukaa muda wote huo bila kocha ni mtihani, tumeanza mchakato wa kumpata kocha mpya lakini kwa sasa timu itakuwa chini ya Kocha Msaidizi, Machupa," amesema Dida

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement