Chelsea imeripotiwa kupiga hodi huko Napoli wakiwafuata na ofa yao ya pesa pamoja na mchezaji ili wamchukue straika Victor Osimhen kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Napoli ilifanikiwa kubaki na huduma ya straika huyo Mnigeria mwaka jana baada ya kuwa na kiwango bora uwanjani na timu nyingi kuhitaji saini yake. Osimhen alifunga mabao 26 kwenye ligi na kuipa timu yake ya Napoli ubingwa wa Serie A.

Osimhen na wachezaji wenzake wamekuwa na wakati mgumu msimu huu na kushuhudia ubingwa ukinyakuwaliwa na Inter Milan, ambapo fowadi huyo mwenye umri wa miaka 25 alishindwa kuonyesha makali ya kufunga.

Maumivu ya misuli ya paja pamoja na fainali za Afcon 2023 zimeripotiwa kumfanya Osimhen kushindwa kuonyesha makali kwenye Serie A, lakini bado mkali huyo amefanikiwa kufunga mabao 16 na asisti nne katika mechi 29 alizocheza kwenye michuano yote.

Fowadi huyo wa zamani wa Lille alikuwa kwenye kiwango bora mwezi uliopita wakati alipofunga mabao matatu katika mechi nne alizocheza kwenye Serie A na kwamba licha ya kusaini mkataba mpya huko Napoli, Desemba mwaka jana, klabu hiyo haina uhakika kama itabaki na huduma yake hadi msimu ujao.

Rais wa Napoli, Aurelio de Laurentiis alishaweka wazi Osimhen ataondoka mwisho wa msimu, licha ya kusisitiza kwamba itabidi kipengele kilichopo kwenye mkataba wake kivunjwe, kwa maana timu inayomtaka ilipe mkwanja usiopungua Pauni 110 milioni.


You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement