Rais wa Barcelona, Joan Laporta amesema klabu hiyo kwa sasa ipo kwenye mazungumzo kwa ajili ya kuwabakiza kikosini mastaa, Joao Cancelo na Joao Felix kwa ajili ya msimu wa 2024-25.

Cancelo na Felix walicheza Barcelona kwa mkopo wakitokea Manchester City na Atletico Madrid mtawalia na baada ya viwango vyao bora kwa msimu wa 2023-24, uongozi wa miamba hiyo ya Nou Camp sasa unafikiria kubaki nao kwenye timu.

Wachezaji hao wawili watalazimika kurudi kwenye klabu zao mama mara tu fainali za Euro 2024 zitakapokamilika, ambapo watakwenda kwenye michuano hiyo ya Ujerumani wakiwa kwenye kikosi cha Ureno.

Hata hivyo, Laporta alisema Barcelona inapambana kwa kila namna kuhakikisha inaendelea kubaki na huduma za wachezaji hao kwa ajili ya msimu wa 2024-25 na lengo kubwa ni kuwaomba tena kwa mkopo kutokana na timu kukabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi.

Felix amekuwa akisakwa na timu nyingi kubwa Ulaya ikiwamo Manchester United ambayo nayo inasuka kikosi chake upya kwa ajili ya msimu ujao.

Barcelona inayokabiliwa na ukata itakuwa na mtihani mkubwa wa kuwabakisha mastaa hao msimu ujao na kuna kila dalili wakaondoka.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement