HAKUNA OFA YA USAJILI ILIYOWASILISHWA KWA STRAIKA WA NAPOLI VICTOR OSIMHEN
Wakati dirisha la usajili la majira ya kiangazi Ulaya likizidi kupamba moto, jina moja ambalo linaendelea kutawala vichwa vya habari ni lile la straika wa Napoli, Victor Osimhen ambaye msimu juzi alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Italia.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Nigeria amejikuta katika wakati mgumu kwa kile kinachoelezwa kwamba hadi sasa hana ofa yoyote ya kueleweka iliyowasilishwa mezani kwa mabosi wa Napoli kwa ajili ya kununuliwa.
Kwa mujibu wa gazeti la Gazzetta, Osimhen ambaye yupo katika orodha ya mastaa wanaowindwa na timu mbalimbali kubwa barani Ulaya kuna uwezekano mkubwa akaendelea kusalia katika timu hiyo msimu ujao. Staa huyu amesaini mkataba mpya hivi karibuni ambao unamwezesha kuondoka ikiwa timu inayomtaka itatoa Pauni 101 milioni, jambo ambalo lilionekana kurahisisha mchakato wake wa kuondoka katika dirisha hili baada ya kufeli lile la majira ya kiangazi mwaka jana, lakini mambo yamekuwa tofauti.
Nyota huyo amekuwa akihusishwa na timu mbalimbali kama Arsenal, Manchester United na Chelsea ambazo ilisemekana kuwa huenda zingetuma ofa kwa ajili ya kumnunua, lakini hadi kufikia sasa hakuna hata moja iliyofanya hivyo.
Mbali ya kushindwa kuondoka kujiunga na timu itakayompa maslahi makubwa na kumfanya apate mafanikio zaidi, pia kuendelea kubaki kwake Napoli kunaiweka timu hiyo katika hali mbaya ya kiuchumi.
Mshahara wa staa huyo kwa sasa ni Euro 10 milioni kwa mwaka akiwa ndiye mchezaji anayelipwa zaidi.
Ikiwa itashindikana kumuuza kwa bei iliyowekwa katika mkataba wake tovuti ya Goal.com imeeleza kwamba, rais wa timu hiyo, Aurielo de Laurentiis amepanga kushusha ili kumuuza.
Mkataba wa Osimhen mwenye umri wa miaka 25 unatarajiwa kumalizika 2026 na msimu uliopita alicheza mechi 32 za michuano yote na kufunga mabao 17.