Kiungo wa zamani wa Yanga anayekipiga kwa sasa Azam FC, Feisal Salum Fei Toto' amekiri kiungo mpya aliyetua kwenye timu hiyo, Shekhan Ibrahim Khamis ni bonge la mchezaji mwenye kipaji na uwezo mkubwa, lakini akamuonya mapema kwa kumtaka ajipange kwelikweli kwa vile ametua katika timu yenye presha kubwa.

Shekhan amesajiliwa na Yanga kutoka JKU na kutambulishwa juzi kwenye mchezo wa Ligi Kuu wakati timu hiyo ikiinyoosha Mtibwa Sugar kwa mabao 4-1, huku akitajwa kama ndiye mrithi wa Fei kwenye kikosi cha Miguel Gamondi akipewa mkataba wa miaka mitatu. 

Akimzungumzia kiungo huyo, Fei alisema ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa na kipaji cha hali ya juu na utamu ni umri alionao, akimtabiria kufanya makubwa na mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara.

"Shekhan ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa na ana kipaji namuona mbali, natarajia atafanya vizuri akipewa nafasi na atapata mafanikio makubwa ndani yake," alisema Fei Toto na kuongeza; "Najua amekuja timu kubwa, anatakiwa kupambana na kuonyesha kile alichonacho bila kujali anaenda kupambana na mastaa gani. Naamini katika kipaji chake muhimu ni kuaminiwa na kupewa nafasi ya kuonyesha kile alichonacho ambacho wamevutiwa nacho na kumpa mkataba"

Alisema hakuna mchezaji ambaye alianza moja kwa moja kuingia kikosini bila mapambano anaamini kiungo huyo akipewa nafasi na akaonyesha uwezo ni hazina kubwa kwa taifa kutokana na kipaji na uwezo mkubwa wa kuchezea mpira alionao.

Fei Toto alisema anamuombea afanye vizuri na apate mafanikio akiwa ndani ya timu ambayo amepata nafasi ya kuitumikia kwa sababu anatamani kuona kipaji hicho kinafika mbali zaidi ya alipo yeye sasa ana anaamini hilo linawezekana.

"Ni mchezaji ambaye nimemshuhudia ni mdogo wangu ameanza kujulikana sasa, lakini ni mchezaji ambaye amekuzwa na kufanywa bora chini ya JKU amepita kwenye misingi ya soka hivyo naamini atakuwa bora na atafanya kile kinachotarajiwa."

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement