AZAM FC Kumnasa Lamin Jarju Kutoka Al Hilal
Dar es Salaam. Mabosi wa Azam FC imefikia sehemu nzuri juu ya kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa Al Hilal, Lamin Jarjou ili kujiunga nao katika unaotarajiwa kufungulia mwanzoni mwa Julai.
Hadi sasa, Azam FC imeshawasajili nyota wawili, Feisal Salum 'Feitoto' kutoka Yanga na Cheikh Sidibe wote kwa mkataba wa miaka mitatu.
Sidibe ni beki wa kushoto ambaye anakwenda kumrithi mikoba ya Bruce Kangwa aliyepewa mkono wa kwaheri, huku Feitoto akiongeza nguvu eneo la ushambuliaji.
Baada ya kukamilisha usajili huo, Azam FC inaaendelea mazungumzo na Jarjou kwa ajili ya kumchukua moja kwa moka badala ya mkopo na wamefikia dau la Dola 250,000 (Sh600 milioni), huku mshahara ukiwa si chini ya Sh50 milioni.
Chanzo kutoka ndani ya Azam FC kililidokeza TV3 kwamba tajiri wa timu hiyo, Yusuf Bakhresa amekataa mchezaji huyo kuja kwa mkopo na badala yake ameona ni bora atumie fedha na baadaye kumuuza.
"Fedha si tatizo, lakini kwenye timu huwa kuna bajeti fulani ambayo haitakiwi kuvukwa, tajiri yupo tayari kukamilisha usajili huu wa Jarjou.
"Kwenye mshahara hapo ndiyo wanazungumza kuona wanamalizana kwa staili ipi, fedha ya usajili inaweza kutoka kwani tajiri yupo tayari kwa hilo ila upande wa mshahara kuna viwango ambavyo ni ngumu kuvivuka."
Pia, chanzo hicho kilisema timu hiyo itasajili kipa mwingine kuziba nafasi ya Wilbol Maseke, kwani utaratibu wao ni kuwa na makipa wanne.
"Maseke kaondoka, wamebaki makipa watatu, kwahiyo itaangaliwa kama inawezekana kipa mwingine akapandishwa au kusajiliwa mpya, ila sehemu kubwa ni kuja kipa mwingine mzawa mwenye uzoefu," kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, Ofisa Habari wa Azam FC amekaririwa na gazeti hili akisema usajili wa wachezaji wao watatangaza hapa nchini na wengine watakwenda kujiunga na timu hiyo nchini Tunisia watakapokuwa wameweka kambi.