Machester City inataka kumtuliza Erling Haaland kwenye kikosi chao wakipanga kumpa dili jipya ili kubaki Etihad kwa muda mrefu.

Haaland ameshinda taji la Ligi Kuu England kwa misimu miwili mfululizo tangu alipotua Man City kwa ada ya Pauni 51 milioni akitokea Borussia Dortmund kwenye dirisha la majira ya kiangazi 2022.

Mkataba wake wa sasa umebakiza miaka mitatu. Kwenye mkataba huo wa sasa, imeripotiwa kuwapo na kipengele kinachomruhusu mchezaji huyo kuondoka kujiunga na timu yoyote nje ya England, ambayo itakuwa tayari kulipa ada ya Pauni 175 milioni kwenye dirisha hili.

Na kiwango cha ada yake ya uhamisho kitakuwa kinapungua kwa kadri mkataba wake unavyozidi kupungua. Na kwa sasa Man City, tayari imeanza maandalizi ya kuishi bila ya kocha Pep Guardiola, ambapo wanaamini Mhispaniola huyo huenda asisaini dili jipya wakati hili la sasa litakapokwisha.

Na kumekuwa na ripoti kwamba hata mkurugenzi wa soka wa klabu hiyo, Txiki Begiristain naye ataondoka kwenye klabu hiyo.

Kutokana na hilo, Man City haitaki kujiweka kwenye presha kubwa na ndio maana imepanga kumpa mkataba mpya Haaland ili azidi kubaki kwenye klabu yao kwa muda mrefu.

Man City imeshinda mataji sita ya Ligi Kuu England katika kipindi cha misimu saba ya mwisho, huku ikiweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya England kubeba ubingwa huo kwa misimu minne mfululizo. Kwenye kikosi hicho cha Etihad, Guardiola, ameshinda pia taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la FA mara mbili, Kombe la Ligi mara nne, Klabu Bingwa Dunia na European Super Cup.

Kuhusu Haaland, mkataba wake wa sasa unashuhudiwa akilipwa Pauni 400,000 kwa wiki.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement