Licha ya kutinga hatua ya makundi, Klabu ya Yanga walianzia nyumbani dhidi ya Manning Rangers ya Afrika Kusini na kutoka sare ya 1-1, huku bao la Yanga likifungwa na Monja Liseki aliyeazimwa kutoka Simba. 

Baada ya mechi hii Yanga wakamfukuza kocha wao Tito Mwaluvanda, aliyewapeleka hatua ya makundi. 

Wakaenda kumchukua kocha wa Rayon Sports ya Rwanda, Raoul Shungu, raia wa DRC ambaye alijipatia umaarufu mkubwa Tanzania kupitia mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, yaliyofanyika Zanzibar Januari 1998.

Kocha huyo aliiongoza Rayon Sports kucheza soka safi na kutwaa ubingwa kwa kuwafunga Mlandege ya Zanzibar 2-1 kwenye fainali. Kabla ya fainali Rayon Sports walikutana na Yanga kwenye nusu fainali na kushinda 3-1.

Kama haitoshi, mwezi Machi, Shungu akakutana tena na Yanga akiwa na Rayon Sports kwenye raundi ya kwanza ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa.

Mechi zote mbili ziliisha kwa sare (2-2 Rwanda na 1-1 Tanzania) na Yanga kufuzu kwa sheria la bao la ugenini. Mpira ambao Yanga walipigiwa mara zote tatu walizokutana na Rayon Sports ya Raoul Shungu, ndiyo uliokuja kuwashawishi baadaye kumchukua kocha huyo raia wa DRC. Kazi yake ya kwanza ikawa dhidi ya Asec Mimosas mjini Abidjan, Septemba 6, 1998. Yanga ilipoteza mchezo huu 2-1 lakini iliupiga mwingi sana na kuleta matumaini kwa mashabiki wake. Mchezo uliofuata ulikuwa dhidi ya Raja Casablaanca huko Morocco, Septemba 20.

Yanga wakatakiwa kutoka Ivory Coast kuelekea Morocco, Jumatano ya Septemba 9, saa sita usiku. Lakini wakakosea kusoma tiketi za ndege...ile saa sita usiku ya Jumatano, wao wakadhani ni usiku wa Jumatano kuamkia Alhamisi, kumbe ni usiku wa Jumanne kuamkia Jumatano. Walipofika uwanja wa ndege wakaambiwa ndege yenu ilikuwa saa sita usiku, yaani usiku wa kuamkia leo..wakachoka. Ndege nyingine ya

kutoka Ivory Coast hadi Morocco ilikuwa Jumatano inayofuata, yaani Septemba 16. Ili kujistiri, wakaenda kuomba kwa wenyeji wao Asec wawape hifadhi kwenye akademi yao hadi ikifika siku ya safari.

Yanga wakapewa hosteli za Asec ambako walikaa na watoto wa akademi. Wakati huo watoto wenyewe ndiyo walikuwa kina Kolo Toure, Aruna Didande, Bonaventure Kalou na wengine wengi ambao baadaye walikuja kuwa nyota wakubwa duniani.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement