Mwezi Mei umekuwa wa kihistoria kubwa kwa nyota wawili wa Kitanzania wanaocheza soka la kulipwa katika klabu tofauti barani Ulaya, Mbwana Samatta na Novatus Dismas baada ya timu zao kufanikiwa kutwaa mataji ya Ligi Kuu katika nchi zilipo.

Nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta alifanikiwa kuvaa medali ya ubingwa wa Ligi Kuu ya Ugiriki baada ya timu yake PAOK kumaliza ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikikusanya pointi 80.

Ingawa Samatta hakupata muda wa kutosha wa kucheza katika kikosi cha PAOK, ameshiriki katika mafanikio hayo kwa kufunga mabao mawili kati ya 87 ambayo timu hiyo imepachika msimu huu katika mbio za kusaka ubingwa huo.

Hilo ni taji la pili la Ligi Kuu kwa Samatta kulitwaa barani Ulaya ambapo la kwanza alichukua katika msimu wa 2018/2019.

Wakati Samatta akifanya hivyo huko Ugiriki, nyota mwingine wa Taifa Stars, Novatus Dismas amefanikiwa kutwaa taji la Ligi Kuu ya Ukraine akiwa na timu ya Shakhtar Donetsk ambalo ni la kwanza kwake la Ligi Kuu barani humo.

Kabla ya hapo, Dismas alicheza katika ligi mbili tofauti barani Ulaya bila kuvaa medali ya ubingwa ambapo kwanza ilikuwa ni Ligi Kuu ya Israel katika timu ya Maccabi Tel Aviv na kisha ligi ya Ubelgiji katika timu ya Zulte Waregem.

Kitendo cha timu za nyota hao wawili kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwenye nchi zao kinawafanya waingie katika orodha ya wachezaji wa Kiafrika ambao wamemaliza msimu vizuri kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na mashindano mbalimbali tofauti ambayo zimeshiriki barani Ulaya huku wengi wakichangia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa mafanikio hayo.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement