VICTOR OSIMHEN SIFA ALIZOZIPATA NIGERIA ZITASOGEZWA KWENYE VIWANGO VIPYA IWAPO ATAISAIDIA KUCHUKUA UBINGWA
Mateso yakizidi jua Neema Inakaribia na Giza lipozidi basi jua kuwa kunakaribia kukucha.
Ndipo hapa tunapomuona Mwanasoka Bora wa Mwaka 2023 wa Bara la Afrika na ni Mfalme mpya wa Soka la Afrika, Victor Osmhen Straika wa Societa Sportiva Calcio Napoli wengi wakiita SSC Napoli lakini pia akilitumikia Taifa lake la Nigeria kunako Timu ya Taifa.
Kama wanasoka wengi mashuhuri Kusini mwa Nigeria, Victor Osimhen alitoka katika malezi duni ya familia.
Wazazi wa Victor wana asili ya familia yao Kusini mwa Nigeria, eneo la Serikali ya Mitaa ya Esan Kusini Mashariki mwa Jimbo la Edo nchini Nigeria na Kabla ya kuzaliwa, wazazi wake walifanya uamuzi wa kuhamia jiji la Lagos Mji mkuu wa kiuchumi wa Nigeria.
Hata wakiwa Lagos, familia yake ilikabiliwa na hali ngumu, Victor wakati huo alikuwa mtoto mchanga ambapo mama yake alikuwa akiuza maji ili kujipatia kipato.
Victor Osimhen amekua pamoja na kaka yake Andrew na ndugu zake wengine wanne huko Olusosun na jamii ndogo karibu na Oregun, Ikeja, Lagos. Jumuiya hii hubeba moja ya jalala kubwa zaidi barani Afrika.
Kwa maana Osimhen amekulia kwenye mitaa yenye vumbi ya Olusosun huko Lagos nchini Nigeria, akilakiwa kila siku na uvundo kutoka madampo au jalala katika mtaa wake, Osimhen anasema alikuwa na hamu kubwa ya kufanikiwa na alifanya kila awezalo kutimiza ndoto aliyokuwa akiikimbiza.
Alilazimika kuuza magazeti na maji ya chupa, ilibidi atembee kwenye misongamano ya magari karibu kila siku ili kustahimili changamoto nyingi ambazo yeye na familia yake walikuwa wanakabiliana nazo.
Shule ya Msingi ya Olusosun, ambayo alisoma Victor ilitumika kama mahali pa mikutano ya mpira wa miguu kwa wanafunzi wote wa shule na vijana katika jamii ya eneo hilo.
Mzaliwa wa kwanza wa familia yao, ambaye jina lake ni Andrew ambaye alitupilia mbali wazo la kujiendeleza kielimu ili apate pesa za kumsaidia mdogo wake ambaye alimkusudia kufanya makubwa kwenye Soka Ulimwenguni.
Victor alijifunza kucheza mpira wa miguu, ndoto zake kubwa ni kuichezea Klabu ya Chelsea FC.
Yeye, pamoja na wanafamilia yake ni mashabiki wakubwa wa timu ya Taifa ya Nigeria (Super Eagles).
Haikuchukua muda kabla ya ndoto ya familia hiyo kuanza kuzaa matunda huku maskauti wa ndani wa soka wakiona kitu cha kipekee kutoka kwa Victor na kisha kumwalika kwenye Ultimate Strikers Academy huko Lagos, ambako alikuwa na majaribio yake ya kwanza na yaliyozaa mafanikio.
Jitihada huzaa mafanikio, mwaka 2014 uwezo wa Victor ulionekana Zaidi na akiwa Ultimate Strikers ulimwona akialikwa na Kocha Emanuel Amunike kuwakilisha timu ya Taifa ya Nigeria iliyochini ya miaka 17 katika mashindano ya Kombe la Dunia l;a FIFA U17.
Timu ya taifa ya Nigeria ya U-17, inayojulikana kama Golden Eaglets, ndiyo timu changa zaidi inayowakilisha nchi ya Nigeria katika soka. Victor Osimhen alisaidia sana timu hiyo kufuzu Kombe la Dunia la FIFA la U-17, ambalo lilifanyika Chile.
Victor Osimhen alianza vyema michuano hiyo kwani alifunga mabao mawili kwenye mechi ya kwanza.
Kando na kuisaidia nchi yake kushinda shindano hilo, Mnigeria huyo mwenye talanta pia alinyakua tuzo ya mfungaji bora zaidi baada ya kufunga mabao 10 na pia Mpira wa Fedha wa Kombe la Dunia la FIFA U-17.
Baada ya Kombe la Dunia, Klabu kutoka Ulaya, kama Arsenal, Man City, na Tottenham Hotspur zilikuwa zikimfuatlia Osimhen, chakushangaza, Victor Osimhen alikataa ofa zote.
Muda mfupi baada ya kutangazwa Mchezaji Bora anayechipukia wa Afrika kwa mwaka 2015 katika Tuzo za CAF mjini Abuja mnamo Januari mwaka2016, Osimhen aliutangazia ulimwengu kwamba angeendeleza taaluma yake katika klabu ya Wolfsburg ya Ujerumani inayoshiriki Bundesliga.
Osimhen alisaini mkataba wa awali wa miaka mitatu na nusu hadi Juni 2020 na akacheza kwa mara ya kwanza katika ligi kuu ya Ujerumani Mei 2017.
Baada ya miezi minne tu ya kucheza Bundesliga yake ya kwanza, matatizo yalianza kumuandama Mnigeria huyo.
Jeraha la bega lilimfanya aende kufanyiwa upasuaji, ambao ulimaliza msimu wake wa kwanza mapema.
Licha ya majeraha aliyokuwa nayo, Osimhen alionekana mwenye matumaini alipokuwa akipambana nchini Ujerumani.
Jinamizi la liliendelea kumuandama Osimhen baada ya kupona jeraha lake la bega, wakati huo, ulikuwa ugonjwa ambao ulimtawala, na kumfanya akose mechi za maandalizi ya msimu mpya na kilichomuumiz Zaidi ni kushindwa kuitwa kwenye Kikosi cha Timu ya Tiaa ya Nigeria kilichoshiriki Kombe la Dunia mwaka 2018 lililofanyika nchini Russia 2018.
Ilimchukua Osimhen takriban misimu miwili wenye maumivu ya kushindwa kutimiza ndoto zake kwa muda alioutarajia, na kwasababu ya jeraha na ugonjwa hakuwahi kufunga bao lolote ndani ya Wolfsburg.
Osimhen aliamua kwenda Unelgiji kwenye majaribio katika Klabu za Zulte Waregem na Club Brugge.
majaribio ya msimu wa joto na vilabu vya Ubelgiji na kulingana na afya yake aligonga mwamba alipougua malaria, ambayo iliathiri hali yake ya kimwili na kufanya klabu zote mbili kumkataa.
Tarehe 22 Agosti 2018 ilikuwa tarehe, Malaika wa soka walimuhurumia, Klabu ya Ubelgiji Charleroi ilimkubali kwa mkataba wa mkopo wa msimu mmoja.
Septemba 22 alifunga bao lake la kwanza kama mtaalamu na kisigino.
Victor Osimhen mwishowe alipata furaha yake baada ya kungojea kwa muda mrefu.
Mnigeria huyo mvumilivu alicheza vyema na timu hiyo ya Ubelgiji, akicheza michezo 36 na kufunga mabao 20, jambo ambalo lilifanya klabu yake, Charleroi, kumnunua akiwa kwa mkopo.
Baada ya kutawala soka nchini Ubelgiji, Mnigeria huyo aliona ni wakati mwafaka wa kurejea kama mshambuliaji mkubwa wa Kiafrika.
Mnamo Julai 2019, Osimhen alisaini Lille OSC ya nchini Ufaransa.
Mabao 18 aliyofunga akiwa Lille yaliifanya Napoli kubisha hodi na hatimaye kuondoka naye na hiyo ikiwa ni mwaka 2020.
Kabla ya msimu wake mzuri ambao alinyakua taji la kihistoria la Serie A, alilazimika kukosa kushiriki Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Afcon2021 kwa sababu ya Covid-19 na jeraha la uso ambalo bado linamhitaji kucheza akiwa amevaa barakoa au kwa Face Mask.
Victor James Osimhen anapambania ndoto zake pamoja na za ndugu zake ikiwa ni sehemu ya shukurani kwa wazazi wake, Baba na Mama ambao walishatangulia mbele ya haki.
Na sasa Yupo Ivory Coast na Timu yake ya Taifa ya Nigeria akipambana kuhakikisha wanabeba Ubingwa wa AFCON2023, Iwapo Osimhen atatwaa taji la Kombe la Mataifa ya Afrika mjini Abidjan tarehe Februari mwaka huu, sifa alizopata nchini Nigeria yenye mapenzi makubwa ya soka zitasogezwa katika viwango vipya Zaidi.