Godfrey Taita beki wa zamani wa yanga ameulinganisha ufundi wanaouonyesha Clatous Chama (Simba) na Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli (Yanga) na alichokuwa akifanya Haruna Niyonzima.

Taita alisema kipindi Niyonzima akiwa kwenye kiwango cha juu, wakiwa mazoezini walikuwa wanafurahia kuona ufundi na kipaji chake, ambapo alikuwa anafanya vizuri hadi kwenye mechi za mashindano.

"Nikiwaangalia Chama, Pacome na Nzengeli namuona Niyonzima fundi ambaye alitufanya hadi wachezaji wenzake tupende kumuangalia anachokifanya mazoezini," alisema nakuongeza;

"Ni nadra mchezaji mwenzako kukaa chini na kuanza kukuangalia unachofanya, lakini enzi hizo Niyonzima alikuwa na ushawishi mkubwa sana na alikuwa hatumii nguvu kama anavyocheza Chama tu, ila alikuwa na akili nyingi nadhani hadi waliokuwa wanamkaba walikuwa wanapata shida naye."

Alisemna mastaa hao kwa sasa wanafanya mpira uonekane rahisi sana kwa aina ya uchezaji wao wa kutumia akili nyingi kuliko nguvu, akisisitiza kuna jipya kwa wazawa kujifunza jambo kwa ajili ya kuibua ushindani zaidi.

"Ukiachana na Niyonzima, wachezaji wazawa ambao nilikuwa napenda kuwaangalia ni Haruna ʻMoshi Boban' Shaban Kisiga, kuna wachezaji wanavitu fulani vya kiufundi ambavyo vitakuvuta tu uwatazame," alisema.

Alisema waliingia msimu mmoja na Niyonzima 2011/12, hivyo walikuwa marafiki wakati mwingine walijadiliana kuhusu kazi. "Jamaa muda wa kazi ni kazi, utani ni utani, kifupi alijua anataka nini ndio maana aliondoka kwa heshima Tanzania."

Taita kwa sasa hachezi mpira waushindani, anafanya biashara za nguo,mabegi akishirikiana na mkewe.

Pacome amecheza dakika 984 kwenye mechi 12 dhidi ya KMC 90, Namungo 67, Ihefu 90, Geita 73, Azam FC 90, Singida Fountain Gate 72, Simba 90, Coastal Union 87, Mtibwa Sugar 30, Tabora United 25, Kagera Sugar 90 na Dodoma Jiji 90, ana mabao manne. Maxi kacheza dakika 973 dhidi ya KMC 17, JKT Tanzania 90, Namungo 90, Ihefu 90, Geita 90, Azam FC 90, Simba 89, Coastal Union 90, Tabora United 90, Kagera Sugar 85, Dodoma Jiji 90, Mtibwa 60, amefunga mabao saba na asisti mbili.

Kwa upande wa Chama ana asisti tatu alizotoa dhidi ya Tabora United mbili na Coastal Union moja.

Niyonzima hadi anaondoka alichukua mataji ya Ligi Kuu sita, manne akiwa naYanga alikocheza 2011-17, na mawili Simba 2017-2019, akaondoka kwenda APR ya Rwanda akarejea tena Yanga 2020/21.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement