Septemba 15, 2025 jijini Tokyo, historia iliandikwa rasmi. Simbu akawa Mtanzania wa kwanza kushinda medali ya dhahabu katika Mashindano ya Dunia ya riadha, akimaliza marathon kwa muda wa saa 2:09:48.


Safari yake haikuwa rahisi. Miaka minane kabla ya ushindi huo, alipohojiwa na BBC baada ya kufuzu kwa mara ya kwanza kushiriki mashindano ya dunia, alisema kwa ujasiri: “naiona dhahabu itakuja.” Kauli hiyo leo imekuwa unabii uliotimia.


Akiwa amechoka baada ya ushindi wake Tokyo, alieleza: “Sikuwa na uhakika wa kushinda, lakini nilipoona mstari wa mwisho karibu nilijisemea lazima nijikaze. Namshukuru Mungu kwa kunipa nafasi ya kuandika historia hii.”


Simbu alizaliwa Februari 14, 1992, wilayani Ikungi mkoani Singida. Alianza kukimbia alipokuwa shule ya msingi, akifanya mazoezi kwa starehe na marafiki zake. Mwalimu wake wa michezo, Madai Jambau, ndiye aliyegundua kipaji chake na kumshawishi akipeleke mbele. Hatua hiyo ilimuweka kwenye njia ya mafanikio makubwa.


Alipofika sekondari ya Winning Spirit, Simbu alianza kuwekeza nguvu zaidi kwenye mbio ndefu, hasa baada ya changamoto za masomo. Hatua ya mabadiliko makubwa ilikuja mwaka 2015, aliposhiriki Gold Coast Airport Marathon nchini Australia na kukimbia saa 2:12:01, rekodi iliyomruhusu kufuzu kushiriki Mashindano ya Dunia Beijing. Tangu hapo safari ya kimataifa ikaanza rasmi.


Tangu 2015, Simbu amewahi kushiriki michuano mikubwa duniani:

  • Beijing 2015 (Mashindano ya Dunia)
  • Rio 2016 (Olimpiki), alimaliza nafasi ya tano
  • London 2017, alinyakua medali ya shaba kwenye Mashindano ya Dunia (saa 2:09:51)
  • Doha 2019, nafasi ya 16
  • Tokyo 2021 (Olimpiki), nafasi ya saba
  • Birmingham 2022 (Jumuiya ya Madola), medali ya fedha
  • Valencia 2024, aliboresha muda wake binafsi (2:04:38)
  • Boston 2025, akashika nafasi ya pili (2:05:04).

Ushindi wa Tokyo 2025 sasa umemuweka rasmi katika orodha ya wakimbiaji wakubwa zaidi duniani. Shirikisho la Riadha Duniani (World Athletics) linamtambua Simbu kama mmoja wa wanariadha 20 bora wa marathon duniani.

Kwa Madai Jambau, mwalimu wake wa zamani, mafanikio haya ni zawadi kubwa: “Nafurahi sana. Nilikuwa namuamsha usiku na wenzake kufanya mazoezi, leo naona matunda yake,” alisema kwa hisia.


Kwa taifa la Tanzania, Simbu amegeuka kuwa alama ya matumaini mapya. Medali ya dhahabu Tokyo 2025 ni uthibitisho kwamba ndoto alizotamka akiwa kijana – “naiona dhahabu itakuja” – hatimaye zimekuwa kweli.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement