KIONGOZI wa zamani wa mapinduzi nchini China, Mao Tse Tung pia wengi wanamfahamu kwa jina la Mao Zedong, alishawahi kutoa kauli moja ambayo inasema, Nguvu zote za kisiasa zinakuja kwa mtutu wa bunduki, huku akiongezea kwa kusema ukiitaka amani itafute kwa nguvu, hata gharama ya damu ihusike.

Wakati nikiendelea kutafakari kauli hii ya mzee Mao, nikaikumbuka kauli yake nyingine ambayo aliwahi kuitamka kwa jamhuri ya watu wa China, aliwaambia wachina wakumbuke kuwa, mbwa anayebweka sana bila mpangilio huyo hakushiba sawasawa.

Ni miaka zaidi ya 100 imepita sasa tangu mzee Mao azungumze na jamhuri ya watu wa China juu ya mambo mbali mbali ya kimapinduzi katika majukwaa tofauti tofauti.

Misemo na falsafa ambazo mpaka sasa zinatumiwa na wachina katika kutengeneza nafasi kubwa kiuchumi baina yao na mataifa mengine.

Wakati Mao akiyasema hayo yote katika karne ya 20 na karne ya 21, matunda ya maneno yanaonekana katika majiji mawili makubwa nchini Uingereza, nchi ambayo imeweza kuchukua nafasi kubwa katika kutengeneza ushawishi mkubwa katika tawi la mpira wa miguu duniani, mimi nimeona niyaandike majina ya London na Manchester.

Ilikuwa ni mwezi wa 6 mwaka 2003, ikiwa ni miaka mitatu tu imepita tangu aweze kuwa gavana wa jimbo la Chukotka Autonomous Okrug nchini Urusi, Roman Abramovich aliingia makubaliano juu ya kununua hisa katika klabu ya Chelsea kwa ada ndogo tu ya kiasi cha Pauni milioni 140 huku akilipa kiasi cha paundi milioni 60 kwanza huku wakikubaliana kumalizia Paundi milioni 80 baadae kidogo.

Roman Abramovich anaingia Chelsea, anamchukua Jose Mourinho kutoka FC Porto mwaka 2004, katika misimu mitatu ambayo anaishi darajani, Chelsea wanachukua mataji mawili ya Premier League, Roman anampatia Mourinho kiasi cha Paundi milioni 70 za usajili.

Timu inawasajili Didier Drogba, Mateja Kezman, Tiago, Michael Essien, Ricardo Carvalho na Paulo Ferreira, Chelsea wanaingia katika utemi mpya na zama mpya za ushindani katika michuano ya Premier League.

Tangu Chelsea iingie kwenye utawala wa myahudi huyu katika kipindi cha miaka 17 iliyopita tayari wana makombe zaidi ya miaka 13 kwenye kabati, hapa ndipo ninapokumbuka maneno ya Komredi Mao kwa watu wa jamhuri ya China, kuwa pasipo kutumia mtutu wa bunduki hakuna amani.

Waulize Chelsea kama wana Premier League, watakwambia wanayo, kuhusu FA wao wanayo, Carabao, UEFA Champions League, UEFA Europa League na uwezo wa kutoa kiasi chochote cha fedha kufanya usajili wa maana, wameingia kwenye maisha ya kutumia mtutu wa bunduki wanaishi kwa amani.

Wakati Roman Abramovic anamalizia muhula wake wa mwisho wa ugavana katika jimbo la Chukotka Autonomous Okrug kule nchini Russia mwaka 2008. Katika jiji la Manchester pale mjini kuna jambo lilikuwa linatokea. Kuna zama mpya zilikuwa zinaanza City Of Manchester.

Tarehe 4 Agosti 2008, kijana mdogo ambaye mara nyingi huwa anapenda kutabasamu aliyekuwa akifahamika kwa jina la Mansour bin Zayed Al Nahyan kutokana na jina lake kuwa gumu waliamua kumuita Sheikh Mansour, alikuwa ananunua hisa pale.

Alitumia kiasi cha Paundi milioni 210 kuchukua wingi wa hisa katika klabu ya Manchester City, Sheikh Mansour anatokea United Arab Emirates, huu ni muungano wan chi za kiarabu. Anatokea nchi ambayo ardhi yake ina utajiri mkubwa wa visima vya mafuta.

Mpaka sasa ametumia zaidi ya kiasi cha paundi Bilioni 1.3 katika kuhakikisha analeta utawala mpya kwenye Premier League, huyu ndiye aliyefanya Manchester Derby ichukua hisia za wengi duniani, huyu ndiye ambaye amekuja kuleta ushindani mpya kwenye jiji la Manchester.

Kuanzia kwenye zama za akina Benjani Mwaruwari, Robinho, Carlos Tevez, Joleon Lescott, Jo, mpaka kwenye zama za akina Yaya Toure, Sergio Aguero, De Bruyne, David Silva na Raheem Sterling, hii ndiyo fahari ya Man City. 

Hapa ndipo kauli ya Komredi Mao Zedong aliyowaambia wachina kuwa ukiona mbwa anabweka sana bila mpangilio huyo hakushiba sawa sawa.

City kwa sasa wanatumia PaunDI milioni 150 kwenye kusajili mabeki, haishangazi, ni maisha yao, maisha ambayo tayari wameshayazoea. Wanatembea mjini wanacheka, wana EPL nne tangu huyu Shehe amekuja pale.

Chelsea na jezi zao za bluu, Man City na jezi zao za bluu, naiona anga ya bluu, naona ndege za Roman Abramovich na Sheikh Mansour zikiwa zinachana mawingu tu. Asante Mao Zedong!

Roman abrahmovch ameondoka Chelsea lakini ameiweka kwenye ramani ya soka duniani tofauti na kipindi ambacho anainunua Club hii yenye mafanikio makubwa kwenye soka la England.

Bila shaka mtu pekee mwenye uwezo wa kuendelea kutekeleza maono ya Mao Zedong ni Sheikh Mansor miongoni mwa binadamu wachache wenye uwezo mkubwa wa kutumia fedha nyingi kwa kuifanya Manchester City kuwa tishio na bora barani Ulaya.

Msemo wa Mao Zedong ni mgumu kama hutatumia muda kuufikiria vizuri kwa kuwa hakuna kitu ambacho amekieleza kwa uwazi bali mengi ameyaongea kwa mafumbo. Tafsiri nyepesi kwa kile ambacho amekizungumza ni uwekezaji

Anatuambia bila kufanya uwekezaji hatuwezi kupiga hatua ndio maana ameamua kutengeneza mifumo mizuri ya uwezekezaji China na kutunufaisha sisi watanzania kwa kutujengea viwanja viwili pale visiwani Zanzibar Na viwanja hivyo ni Mao Zedong one na two

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement