Mchezaji mmoja alikosekana wakati wa michezo miwili ya kwanza ya Zambia kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika 2023, lakini kutochaguliwa kwa Enock Mwepu hakukuwa na uhusiano wowote na uwezo wake.

Badala yake, ni kwa sababu kiungo huyo, ambaye alikuwa nahodha wa nchi yake katika mechi mbili za kwanza za kufuzu mwezi Juni 2022, alilazimika kustaafu soka baada ya kugundulika kuwa na ugonjwa wa moyo.

Wakati huo, mnamo mwezi Septemba akiwa na miaka 24, aliugua nchini Mali na akafanyiwa vipimo aliporejea katika iliyokuwa klabu yake, Brighton ya Ligi Kuu ya Uingereza, na kupokea matokeo hayo mabaya zaidi ambayo hakuwahi kufikiria.

Seagulls walisema Mwepu atakuwa katika "hatari kubwa sana ya kupatwa na mshtuko mbaya wa moyo" ambayo inaweza kusababisha hata kifo ikiwa ataendelea kucheza.

"Ni pigo kubwa kwa Enock, lakini anapaswa kuweka afya yake na familia yake mbele," mkuu wa masuala ya tiba wa Brighton alisema wakati huo.

"Hili ni chaguo sahihi, ingawa ni vigumu kuacha mchezo anaoupenda."

Hata hivyo si uamuzi ambao wanasoka wote wa Afrika katika nafasi ya Mwepu wangefanya.

Miezi miwili tu iliyopita, mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Ghana Raphael Dwamena alifariki dunia baada ya kuanguka uwanjani nchini Albania, alipochagua kucheza baada ya kutoa kifaa cha kupandikizwa cha kufuatilia mapigo ya moyo kila mara yaani cardioverter-defibrillator (ICD), kilichowekwa mwaka 2020, ambacho kingeweza kuzuia mshtuko wake mbaya wa moyo.

Kiungo wa kati wa Manchester United Christian Eriksen aliwekewa kifaa kama hicho baada ya kuzimia alipokuwa akiichezea Denmark kwenye michuano ya Euro 2020.

Moja ya vilabu vya zamani vya Dwamena, FC Zurich, iligundua matatizo ya moyo wake kwa mara ya kwanza mwaka 2017 na kushauriwa na wataalam mbalimbali na madaktari wa magonjwa ya moyo kwamba angeweza kuendelea - jambo ambalo alifanya - huku timu hiyo ya Uswisi Super League ikihakikisha kila mara ina kifaa cha kufanya moyo upige tena wakati akiwa uwanjani iwapo kutatokea dharura.

Lakini hakukuwa na kipengele kama hicho katika klabu ya Egnatia FC ya Albania, ambao hawakupata mawasiliano lakini wakaiambia Athletic mwaka jana kwamba walikuwa na furaha kwa Dwamena kucheza "ili mradi majaribio yote yalifanywa na klabu".

Cha kusikitisha ni kwamba mshambuliaji huyo wa zamani wa Black Stars hakuwa Mwafrika pekee aliyefariki uwanjani mwaka jana.

Moustapha Sylla alifariki dunia Machi mwaka jana alipokuwa akiichezea timu ya Racing Club d'Abidjan ya Ivory Coast, nchi ambayo kwa sasa ni mwenyeji wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika inayoendelea.

Kama Dwamena, Sylla pia angefahamu kwamba alikuwa akihatarisha maisha yake kwa kuingia uwanjani, kwani beki huyo alitolewa katika ligi ya Mali mnamo 2022 baada ya uchunguzi wa lazima wa kiafya kabla ya msimu mpya kufichua hali yake.

Kifo chake, akiwa na umri wa miaka 21 tu, kilimsukuma nahodha wa zamani wa Ivory Coast Didier Drogba kutoa ombi kwa niaba ya wachezaji wote wa ligi ya ndani ya nchi yake baada ya kutokea kwa kifo cha tatu kutokana na ugonjwa wa moyo tangu 2019.

"Rambirambi kwa soka la Ivory Coast vifo 3 vya wachezaji katika ligi kuu ya Ivory Coast katika muda wa chini ya miaka 4…," Drogba alichapisha ujumbe huo kwenye mtandao wa X, wakati huo ukijulikana kama Twitter.

"Ni lini kutakuwa na uchunguzi wa lazima wa kiafya kwa wachezaji "wataalamu"?... Kipimo cha damu, ECG [Echocardiogram], vipimo vya msongo wa mawazo? Dawa kwa ajili ya wachezaji zitafika lini?"

Huku takriban wanasoka zaidi ya 10 wa Kiafrika wakijulikana kufariki kutokana na matatizo ya moyo kwa miaka mingi, mtazamo wa Drogba kuhusu kuhitaji masharti magumu zaidi ya matibabu kwa ajili ya matatizo ya moyo ni moja ambayo nyota mwingine wa zamani wa Chelsea anakubaliana nayo.

"Nilicheza Ulaya mara kadhaa na ninajua kuwa unaposaini mkataba, lazima upite mchakato wa matibabu," Geremi, mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Cameroon ambaye sasa ni mwakilishi wa chama cha wachezaji.

"Tunapaswa kutekeleza hilo hapa Afrika."

Ingawa hii hutokea katika baadhi ya vilabu vya Afrika, haifanyiki kote - sababu moja ya ombi la Drogba.

Kama vile Geremi, ambaye alimpoteza mchezaji mwenzake Marc-Vivien Foe uwanjani mwaka wa 2003, Drogba pia alimpoteza mchezaji mwenzake wa kimataifa kutokana na tatizo la moyo. Cheick Tiote, bingwa wa Afrika mwaka 2015 ambaye alikuwa naye uwanjani mara kadhaa.

Suala moja kuu ni kwamba moyo wa Kiafrika unaaminika kukabiliwa zaidi na matatizo ya moyo, huku timu ya utafiti wa kimatibabu ikiungwa mkono na shirikisho la soka duniani Fifa, mwaka 2009, ikiamua kwamba "wanariadha weusi wa Kiafrika wanaonekana kuwa na hatari kubwa ya kupatwa na magonjwa ya moyo wakati wa matukio ya michezo".

Suala lingine la msingi ni kukataa kwa baadhi ya wachezaji wenye matatizo ya moyo kutii ushauri wa matibabu.

Daktari wa Afrika Kusini Lervasen Pillay ni mtu ambaye anajua hili vizuri sana, baada ya kuwashauri wanasoka watano tofauti kuacha kucheza kwa sababu ya matatizo yanayohusiana na moyo.

"Sio mazungumzo rahisi kamwe, kwa sababu mtu amekuwa akifanya kazi hii kwa miaka 10-15 na sasa umempa habari ya kusema, 'Sikiliza, huwezi kufanya hivi tena, unahitaji kuwa na mpango mwingine wa maisha', " Dkt Pillay.

"Wachezaji kandanda wengi hawajaanzisha Mpango Mwingine wanapokuwa na umri wa miaka 25, na mazungumzo mara nyingi yanatokana na swali hilo kamili: 'Nitafanya nini ikiwa nitaacha kucheza soka?'

Kwa Dk Pillay, ni vigumu kutazama wakati wachezaji ambao wameambiwa wasicheze bado wanashikilia Mpango wao wa awali wa kuingia uwanjani licha ya kujua hatari inayowakodolea macho.

"Unapoona jina la kijana huyo kwenye kikosi cha wachezaji wanaoanza kucheza unashtuka - na ikiwa itakuwa mechi ya kutazamwa kwenye televisheni, nitabadilisha chaneli," alisema.

Mgonjwa mmoja, ambaye jina lake haliwezi kutajwa bila kukiuka sheria za usiri, alifariki miaka miwili baada ya kushindwa kumsikiliza Dk Pillay, na kumwacha na "huzuni kwa muda".

"Ukipata mtu mwenye tatizo la moyo, basi hakikisha huduma yake ya matibabu inakuwa karibu ili uwe na vitu kama vile Kifaa cha kufanya moyo uanze kupiga tena, ufikiaji wa hospitali kwa haraka na magari ya dharura, kwa sababu kama huna, unatafuta matatizo."

Wakati FC Zurich ilichukua hatua hiyo haswa kuhusiana na Dwamena, vilabu vingine vingi havijafanya hivyo.

Kumekuwa na matukio ya kukumbukwa hapo awali ambapo masharti ya kimsingi ya matibabu hayakupatikani katika viwanja vya kucheza vya Waafrika, kama vile wakati mwanasoka wa ndani wa Nigeria Chineme Martins alipofariki mwaka wa 2020 kufuatia kushindwa kupatikana kwa matibabu.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement