KOLO TOURE: NIGERIA NA IVORY COAST FAINALI HII ITAKUWA MECHI KALI ZAIDI
Baada ya rekodi ya idadi ya mabao kufungwa, kuwapata wababe wa Afrika na vilevile viwango vilivyoshuhudiwa vya sarakasi na msisimuko, Makala ya hivi punde ya michuano ya bara Afrika AFCON yanafunga jamvi usiku huu wakati ambapo wenyeji Ivory Coast watakabiliana na mabingwa wa zamani Nigeria, kusaka taji la bingwa wa Afrika.
‘Super Eagles’ ya Nigeria ikitafuta ushindi wao wa nne barani, jijini Abidjan huku wenyeji Ivory Coast wakitafuta ushindi wa tatu baada ya ule wa 1992 na 2015.
Timu hizo zitakutana kwa mara ya pili, katika Makala haya yaliyoandaliwa Ivory Coast , siku 24 baada ya Ivory Coast kucharazwa bao moja kwa nunge na Nigeria nyumbani katika awamu ya makundi.
Timu ya Elephants ndio wenyeji wa kwanza kufika fainali katika mashindano ya Afcon, tangu Misri ilipoandaa mashindano hayo 2006, huku wenyenji watano kati ya sita walioshiriki kwenye fainali hizo kunyakuwa taji hilo, isipokuwa Super Eagles 2000.
Nigeria ambayo haijafungwa na kwa sasa inaorodheshwa juu miongoni mwa timu zilizofikia fainali.
Nigeria ni nambari sita barani Afrika na 42 ulimwenguni wakilinganishwa na Ivory Coast ambao wanaorodheshwa nambari 8 Afrika na 49 ulimwenguni.
Nigeria inayosaka taji lake la kwanza tangu 2013, Super Eagles waliingia katika fainali bila ya tatizo , walijinyakulia pointi saba kwenye kiwango cha makundi, na kuwafunga Cameroon, Angola na Afrika Kusini kwenye raundi ya 16 bora.
Na kwa upande wao, baada ya kupokea kichapo kutoka Nigeria, Ivory Coast walipata kichapo kingine kutoka kwa Equitorial Guinea cha mabao manne kwa nunge, na kupita kwa shimbo jembamba kama timu ya tatu bora . Walipoingia raundi ya 16 bora, waliinuka na nguvu mpya walipoiondoa mabingwa watetezi Senegal na kuishinda Mali kabla ya kucharaza Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwenye robo fainali.
Baada ya Makala bora zaidi kushuhudiwa katika siku za hivi karibuni, matumaini ni kwamba fainali ya usiku wa leo jijini Abidjan kwenye uwanja unaojaa watu 60,000 utakuwa na msisimko mkubwa.
‘Maandalizi yamekuwa murua kabisa, viwanja ni vizuri na mechi tulizoshuhudia zilikuwa bora kabisa, na sasa Nigeria inakabiliana na Ivory Coast katika fainali – Itakuwa mechi kali, ‘ amesema mchezaji wa zamani ya timu ya ‘Ndovu’ Kolo Toure.