KELVIN CHERUIYOT KIPTUM AMEACHA ALAMA ISIYOWEZA KUFUTIKA
Ilikuwa Disemba 02 Mwaka 1999 katika kijiji cha Chepsamo huko Chepkorio, kilipata Mwanga ambao hawakujua kama baadaye utakuja kuwaangazia na kukuza zaidi jina la eneo Hilo.
Ni kilomita 30 kutoka Eldoret katika Bonde la Ufa likiwa maarufu kama ardhi ya mabingwa,
Wanariadha wengi wa Kenya wanatoka eneo hilo.
Naam, ni nchi ya Kenya ambapo alizaliwa Shujaa, nyota, Mwanamichezo wa ajabu aliyeweza kuacha alama isiyoweza kufutika Duniani, ni Mshindi wa rekodi ya dunia ya mbio za marathon za wanaume, Kelvin Cheruiyot Kiptum
Kaka ilivyo kwa jamii nyingi za watu kutoka nchini Kenya, vipaji hurithiwa, hususani katika mchezo huu wa Riadha ambao Kenya umejizolea umaarufu Mkubwa Sana kwa kuzalisha wanariadha walioweza kuweka rekodi kadha wa kadha kama Paul Kibii Tergat, Moses Kiptanui, Brimin Kipruto, Ezekiel Kemboi na wakina Eliud Kipchoge.
Kelvin Kiptum alizaliwa familia ya vipaji kwani mama yake alikuwa mchezaji wa mpira wa wavu huku Baba yake mzee Samson Cheruiyot akiwa ni mwanariadha wa zamani.
Licha ya Elimu aliyoipata pale St Patrick High School lakini Kiptum alifanya kazi katika shamba la mifugo la familia yake katika ujana wake kama ilivyo kwa jamii nyingine za watu wa Kenya.
Alianza kukimbia akiwa na umri wa miaka 13 akiwa na lengo Moja Kubwa la kutimiza ndoto aliyojiwekea.
Kama ilivyo kwa wanamichezo wengine wenye kutazama zaidi njia ya mafanikio, akiwa na umri wa miaka 13 Kiptum aliingia katika nusu marathon yake ya kwanza kwamaana ya Eldoret Half Marathon na kushika nafasi ya 10 kwa ujumla.
Miaka mitano baadaye, mnamo 2018 akiwa na umri wa miaka 18, alishinda mbio hizo.
Alishiriki shindano lake la kwanza la kimataifa mnamo 2019 akiwa bado kijana wa umri wa miaka 19 , na alitumia muda wa Dakika 59 na sekunde 54 kumaliza akishika nafasi ya tano kwenye Lisbon Half Marathon.
Katika kuhakikisha anafikia mafanikio na jina lake kuweza kubwa zaidi Nchini Kenya, Afrika na Duniani, Kiptum akiweza kuboresha zaidi muda wake katika Riadha kwani katika mbio ambazo aliendelea kushindana kwamaana ya Half Marathon Kiptum akiweza kutumia Dakika 58 na sekunde 42 katika Valencia Half Marathon ya mwaka 2020.
Kati ya 2019 na 2021, Kiptum alivunja rekodi ya dakika 60 kwa nusu marathon mara sita.
Aliendelea kufanya makubwa zaidi katika umbali mrefu na kama ilivyokuwa 2022 aliooshindana mbio za Valencia Marathon.
Kiptum aliandika historia kwa kutumia muda wa kasi zaidi kuwahi kutokea kwa mchezaji wa kwanza wa mbio za marathoni akitumia saa 2 na sekunde 53 akielekea ushindi.
Alithibitisha kuwa ushindi wake nchini Uhispania haukuwa wa kusuasua alipotumia saa 2 na sekunde 25 na kushinda mbio za London Marathon mwezi Aprili, wakati huo ilikuwa mara ya pili kwa kasi zaidi katika mbio za marathon za wanaume.
Kiptum alifika kilele cha mbio za barabarani alipofikisha rekodi ya dunia ya saa 2 sekunde 35 kwenye mbio za Chicago Marathon ikiwa ni Oktoba mnamo mwaka 2023.
Mwezi Oktoba mwaka uliopita, Kiptum aliweka rekodi mpya ya kuwa mwanariadha mwenye kasi zaidi katika historia ya mbio za masafa marefu.
Alimaliza mbio za Chicago Marathon kwa muda huo sekunde 34 tu kutoka kwa rekodi ya awali iliyokuwa ikishikiliwa na mwanariadha mahiri Eliud Kipchoge mjini Berlin mwaka 2022 baada ya kukimbia kwa saa mbili, dakika moja na sekunde tisa.
Kiptum, ambaye mbio zake zilizofuata zilikuwa Rotterdam Marathon mwezi wa Aprili, alipaswa kuwa moja ya vivutio vya nyota katika Michezo ya Olimpiki ya majira ya joto huko Paris, Ufaransa baada ya kutajwa katika kikosi cha Timu ya Kenya cha marathon kwa wanaume kwa michezo hiyo.
Mnamo Februari 11 mwaka huu wa 2024, Jua lilizama na makali yake, ajali ya gari ikakatisha safari yake ya hapa Duniani akiwa na miaka 24, akiacha rekodi mpya iliyoidhinishwa wiki Moja iliyopita na Shirikisho la riadhaa duniani kwa maana ya IAAF ya kuwa mwanariadha mwenye kasi zaidi katika historia ya mbio za masafa marefu Duniani.
Kiptum alifariki dunia pamoja na kocha wake, Mnyarwanda Gervais Hakizimana katika ajali mbaya ya barabarani Jumapili usiku huku abiria mwingine mmoja akipelekwa hospitalini akiwa na majeraha mabaya.
Kenya, Afrika na Dunia nzima inakulilia, Tumepoteza Shujaa wa kutaifa, Afrika na wa Dunia..... Tunamaini Familia yako ukiwa umeacha mke na watoto wako wawili watayaenzi yote mema uliyoyaacha hususani katika Tasnia ya Michezo.
Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea.
Raha ya milele umpe ee Bwana, na mwanga wa milele umuangazie, apumzike kwa amani....