USIKU wa tarehe 4, Oktoba mwaka 2006 pale mji mkuu wa Slovenia, Ljubljana, bodi na baraza la shirikisho la soka barani Ulaya, UEFA walikaa chini kutafuta viwanja ambavyo vitakuwa vinaongoza fainali zitakazofanyika miaka ya 2007/08 na 2008/09.

Viongozi hawa walikuwa wanajadili namna ya kupata viwanja vizuri kwa ajili ya kuongoza fainali zinazofuata, huku wakiangalia mambo mbali mbali kama ujazo wa uwanja, usalama na upatikanaji wa vitu.

Moja ya viwanja vilivyotajwa ni pamoja na Estadio Olimpico wa pale Sevilla, Olyimpiastadion wa pale Berlin, Wembley London, Stadio Olimpico pale Roma bila kulisahau jina la Luzhniki Stadium uliopo jiji la Moscow nchini Russia ambao uliteuliwa kuongoza fainali za 2007/08.


Luzhniki Stadium ulitumika mwaka 1999 kwenye mchezo wa UEFA Cup Final ambapo Parma ya Italia iliinyoosha Olympique Marseille ya Ufaransa mabao 3-0.

Safari hii, uwanja huu ulikuwa una kazi ya kuvumilia maumivu mengine kutoka kwa vidume wawili kutoka katika majiji mawili makubwa nchini Uingereza ambapo Jiji la London lilikuwa linakutana na jiji la Manchester. Manchester iliwakilishwa na Man United, London ikawakilishwa na Chelsea.

Ilikuwa inasubiriwa siku ya tarehe 21 mwezi mwei mwaka 2008, tayari tiketi zilikuwa zimeshaanza kuuzwa kama kawaida kwenye platforms zote za kawaida na za mtandao wa UEFA.com. 

Tiketi zilikuwa katika madaraja matatu tofauti, zilikiwa zile za Euro 80, euro 140 na euro 200. Klabu zote mbili zilikuwa zimeshauza zaidi ya tiketi 42,000 huku pia kukiwa na zaidi ya mashabiki 25,000 ambao wangesafiri kutokea nchini Uingereza kwenda nchini Urusi kutazama fainali hiyo. 

Lakini mashabiki hao hawakuweza kwenda kutokana na sababu mbali mbali za utaratibu wa nchi ya Urusi kama zilivyobainishwa na Mikhail Ignatiev ambaye alikuwa ni afisa wa maswala ya kitalii kipindi hicho. 

Mauzo ya tiketi yalikamilika hivyo, ilikuwa ni uwanja wenyewe ushindwe kubeba mashabiki 69,500 ambao hata hivyo walikuwa ni wachache kwani uwanja ulikuwa una uweza kwa kujaza binadamu 85,000.

Kuna wahenga wawili nahisi walikuwa wanadaiana hapo zamani, walisema usiku wa deni haulali, nadhani hapa walikuwa sahihi. Siku ya jumatano tarehe 21 ikafika. Na ilikuwa lazima ifike, hata kama ingechelewa kiasi gani.

Mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 40, kutokea nchini Slovakia aliyekuwa anafahamika kwa jina la Lubos Michel ndiye aliyeteuliwa kuamua mbivu na mbichi kwa kuwa mwamuzi wa kati.

Kwa mara ya kwanza ilikuwa nchi ya Slovakia inatoa mtu wa kusimamia fainali kubwa ya Ulaya hivyo Lubos alikuwa na wasaidizi wake Roman Slysko, Martin Balko na fourth official akiwa ni Vladmir Hrinak.

UEFA hawakuwa na shaka na Lubos Michel kwani ni mtu ambaye alikuwa na uzoefu mkubwa, kuongoza zaidi ya mechi 55 katika michuano ya UEFA, huku akiwa ni mzoefu wa kuongoza michuano mingine kama OLimpiki na kombe la dunia.

Hali ya hewa ikiwa ni Humidity 96, kama kawaida ya nchi ya Urusi. Tayari mambo yalikuwa safi kabisa kuhakikisha yupi ambaye atasukwa na yupi ambaye atakubali kupiga upara.

Gozi la ng'ombe lilikuwa kama kawaida limetoka kwa wataalam wa kazi Adidas, waliamua kuupa jina la Adidas Finale Moscow, mpira huu ambao siku chache pale Manezhnaya ulizinduliwa na David Taylor, Franz Beckenbauer na Vitaly Mutko.

Mashetani wekundu kama kawa uzi mwekundu na mweupe, golini amesimama Edwin van der Sar, kulia mpole wa darasa Wes Brown, kushoto Patrice Evra, katikati ni Rio na Nemanja wakamaliza, mbele yao walisimama wastaarabu Paul Scholes na Michael Carrick, kulia Owen Hergeaves, kushoto bishoo Cristano, katikati Rooney na Tevez. 4-4-2 hiyo.

Wanangu wa darajani, uzi wa samawi kama kawa. Petr Cech kwenye mchuma, kulia mtu wa kazi Essien, kushoto Arsenal wa jana, Chelsea wa leo, Ashley Cole, kati kati Carvalho na kaka mkuu Terry, mbele kidogo Makelele, mjerumani halisi Ballack, muingereza chuma Lampard, fundi Joe Cole kulia, kushoto Malouda, kati Drogba.

Ukiangalia vikosi, utaona vilikuwa kimbinu zaidi hasa kikosi cha Avram Grant, aliamua kumuanzisha Michael Essien mbavu ya kulia badala ya Paulo Ferreira ambaye hata kwenye michezo ya nusu fainali hakuanza, pia akimuanzisha Florent Malouda badala ya Solomon Kalou.

Kwenye vyumba vya matangazo walikuwa wataalam wa kazi kutoka ITV 1 kama Steve Rider, Clive Tyldesley, David Pleat kama mchambuzi, Andy Townsend na Mark Hughes, kutoka Sky Sport alikuwepo Richard Keys, Graeme Souness, Jamie Redknapp, Ruud Gullit kwa njia ya simu, matangazo yakirishwa na Martin Tayler na Andy Gray.

Dakika ya 21, Paul Scholes anapata majeraha ya kutokwa damu puani baada ya kugongana na mtu mweusi Claude Makelele.

Dakika tano baadae, wapole wa darasa Paul Scholes na Wes Brown wanafanya fujo moja ya nipe nikupe, Scholes anampa Wes Brown, Wes Brown anatazama alipo Ronaldo, anamimina krosi moja kutoka kulia, yule mtoto wa kireno Ronaldo anaruka kama anatembea vile. Cech anauangalia mpira, tayari waya huko. Walete.

Tukiwa tunaendelea kufanya mahesabu, tayari watu wa darajani wamekaza meno kweli kweli, dakika ya 45 kipindi cha kwanza, Essien anaachia kombora ambalo linazuiwa na Vidic na Ferdinand. 

Jezi namba 8 bora ya muda wote Chelsea inawarudisha wana London mchezoni, Lampard anawaambia, hii ni fainali wazee. Ngoma 1-1 hiyo. Ananyoosha mikono juu kumkumbuka mama yake ambaye alifariki mwezi mmoja uliopita.

Dakika 45 za kipindi cha kwanza zinakamilika, hakuna mbabe kila mmoja anaingia vyumba vya kubadilishia nguo akiwa, Ferguson amekasirika, Grant anawaaita vijana wa Chelsea ambao muda huo wana morali.

Kipindi cha pili, Chelsea walikuja na moto, Michael Essien anataka kuwainua wanadarajani dakika ya 54, baadae dakika ya 77, Didier Drogba anataka kuwainua wanachelsea tena lakini mambo yanakwenda kushoto.


Baada ya dakika zote 120 kumalizika huku wanamanchester na wanalondon wakiwa wanasubiri hatima yao, ilibidi Pilato atoe hukumu ya penati hivyo hapa kufa kwa mmoja ilibidi iwe lazima na shuruti bila hivyo mwali asingeenda popote.

Wakati huo jiji la Moscow tayari manyunyu ya mvua yanaendelea kumiminika kwenye ardhi ya Moscow, kura ya kupiga penati ikawangukia wana United, Carlos Tevez anaanza vizuri, Michael Ballack anawaleta wanachelsea.

Michael Carrick analipiza, Belleti na yeye anawarudisha wana mchezoni, mwanangu Ronaldo anawapeleka wenzake makosa, namuona analia machozi pale lakini maji ya mvua yanapita na machozi. 

Kama kawaida yake Lampard anawaleta wana tena, 3-2 hiyo inasomeka Owen Hergeaves anaweka kambani, Ashley Cole analipiza, wakati Luis Nani anafanya mambo kuwa 4-4, John Terry anawanyima wanachelsea mwali, wakati anakwenda kupiga ile ngoma, Der Sar alikuwa ameshajiuza. Terry anateleza, ngoma imelala. 

Anderson anawaongezea nguvu watu wa Manchester, Kalou anasawazisha kibarua, mzee wa leo, kijana wa jana, Ryan Giggs anafanya ubao usomeke. Sasa ikawa ni Nikolas Anelka achague mawili, kuwainua wanalondon au awauze kama alivyowauza Terry.

Anelka alichagua mwenyewe kuwauza wenzake, Moscow inalipuka kwa shangwe, kombe linaandikwa Manchester United. Ubingwa wa tatu wa UEFA, Ballack atafanya nini sasa zaidi ya kulia, Terry machozi yako hayasaidii, na mvua ile ni kama machozi ya samaki baharini.

Glory Glory Glory Man United! United, United, United!

Kwa bahati mbaya kwa msimu huu timu zote hazielezeki, hakuna hata moja ambayo inaweza kutikisa tena Ulaya kama kipindi kile.

Chelsea ya Mautio Porchtino bado ina ungaunga pamoja na Manchester united pengine tuendeleee kusubiri ipo siku tutaziona zikirudi tena kwenye ubora.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement