FAINALI YA EURO 2012 IKER CASILLAS ALIMUOMBA XAVI WAPUNGUZE UKALI WA KUSHAMBULIA LANGO LA ITALY
Italy wanapigwa 4-0 ndani ya Kyiev Ukraine. Wameshindwa kabisa kujibu maswali magumu wanayoulizwa na Hispania.
Watafanya nini mbele ya watoto wanaowaka moto mguuni? Katikati yupo Sergio Busquets, Xavi Hernandez, David Silva na Xabi Alonso. Utawaambia nini? Hapo Andres Iniesta amesogezwa mbele, Italy wamedanganywa ni mshambuliaji.
Watoto wa Hispania hawaelewi kitu, wanapika tu sambusa uwanjani. Wanagonga tu. Hiyo Hispania, acha kabisa.
Hispania walikuwa na kiburi cha binadamu mmoja katikati ya dimba aliyezibeba akili zao, akaibeba falsafa yao na akabeba ramani yao.
Alipiga pasi zaidi ya nusu za pasi walizopiga Italia. Bado alitoa assist mbili. Alikuwa kitanzi kwenye shingo ya Italia. Sorry, namzungumzia Xavier Hernandez Creus.
Baada ya bao la Juan Mata, Ilibidi Iker Casillas asogee hadi katikati ya uwanja kuwaombea Italy msamaha.
Casillas akamnong'oneza Xavi, "Hii ni Italy, mabingwa wa dunia mara nne, isitoshe wana Andre Pirlo katikati ya uwanja na gwiji Gianluigi Buffon langoni, sitataka kuwaona wakifungwa tano, tafadhali inatosha. Wasimamishe vijana". Hiyo ndio ikawa 'pona' ya Italy.
Usisahau hiyo ni fainali ya 'EURO 2012', Italy wanaitetea tena kwa mara ya pili. Ni hapahapa Kyiev walivunja rekodi ya kupiga pasi nyingi katika mchezo mmoja.
Wakati wanawakung'uta Ireland katika mchezo wa makundi, Hispania walipiga pasi 857, Xavi na rafiki yake Iniesta wakipiga nyingi zaidi ya timu nzima ya Ireland.
Iniesta akawa mchezaji bora wa mashindano, ila Xavi alikuwa mchezaji bora mashindano yaliyopita ya 2008.
Wakabadilishana tuzo kama walivozoea kubadilishana namba za jezi. Vaa nane klabuni, mimi niivae timu ya taifa. Wale watu.
Muulize hata Frank Lampard anawajua. Alipoulizwa kiungo mgumu kuwahi kukutana nae, alishindwa kuchagua akasema tu Xavi na Iniesta.
Sijui yupi mgumu zaidi, ila hao wawili. Sijawahi kuona wachezaji wanaoelewana uwanjani kama wao.
Huwezi kuwasogelea, huwezi kuwakaba, huwezi kuwakimbia, wanakuchanganya tu. Hadi sir Alex Ferguson analijua balaa lao. Wakati Barca wanampiga 2011. Hadi Sir. Alex Ferguson alinyoosha mikono juu na kukiri kwamba amewashindwa. Wakati Barcelona wanaibutua Man United katika fainali ya UEFA mwaka 2011 pale Wembley, shoka Iniesta na mpini wake Xavi walimsimamia kooni. 'Big g' zake zikawa chungu.
United walipiga shuti moja tu lilolenga lango, walikuwa na umiliki wa mpira wa asilimia 33 tu. Walizidiwa kila kitu na Barca kasoro kadi na rafu tu.
Baada ya mchezo Fergie alisema "Sijawahi kucheza na timu ngumu kama hii.
Timu iliyokamilika kila eneo kama hii, sijawahi kuiona. Sijawahi kukutana na viungo wanaoelewana kama hawa.
Kuna muda nilidhani wachezaji wangu wataanguka kwa kizunguzungu kwa namna mpira ulivokuwa unazunguka.
Yule Xavi na Iniesta walitushinda ujanja kabisa." Kumbuka hapo Barca walikuwa wanaipiga United kwa mara pili mfululizo katika fainali ya UEFA.
Kwasababu tupo na Xavi leo, tumuache huyu ndugu yake.
Tutamrudia Iniesta siku nyingine. Xavi yeye alifika Barcelona mapema sana, akiwa na miaka 11 tu alijiunga na 'La Masia'.
Kwasababu alitokea katika familia bora kifedha, hakuwahi kulazimishwa kwenda shule. Wazazi wake walimshauri aweke nguvu zaidi kucheza mpira kuliko kusoma, walimuona akifanikiwa zaidi ndani ya uwanja kuliko darasani. Wakampeleka La Masia akaanze maisha ya soka.
Alikulia hapo akizitazama sana mechi za kingereza.
Yeye mwenyewe anadai kuwa analihusudu sana soka la Paul Scholes. Basi akakulia katika academy ya La Masia. Alipokuwa na miaka 19, AC Millan walitaka kumsajili.
Wakamuahidi mshahara mrefu na nafasi katika timu ya kwanza. Kumbuka enzi hizo AC Millan wanatesa Ulaya. Xavi alikuwa tayari kupokea hiyo ofa, baba yake vilevile alikubali.
Ila mama yake alimuambia akiondoka Barcelona atavunja ndoa na baba yake. Waachane. Basi Xavi kwa kuiheshimu ndoa ya baba akaamua kubaki Barca.
Ni mume wa Nuria Cunirella, msichana aliyemgombania na Carles Puyol mwaka 2012. Puyol aliachana na mpenzi wake ili awe na Nuria, ila Xavi alimzunguka na kumpata Nuria.
Walipofunga ndoa 2013, wachezaji wengi wa Barca walihudhuria ila Puyol hakuwepo Mpaka leo inadaiwa hawana mahusiano mazuri. Mapenzi bwana!