MARA ya mwisho Yanga kufanya walichokifanya, Benjamin William Mkapa alikuwa katika awamu yake ya uongozi wa nchi hii. Clement Mzize alikuwa hajazaliwa. Ndio, Waingereza walikuwa bado wanakishikilia kisiwa cha Hong-Kong.

Na wamefanya hivyo kwa mbwembwe nyingi. Mbwembwe kubwa za kuiita siku yenyewe ‘Pacome Day (Kitaalamu Zaidi)’. Mashabiki na wachezaji wao wakapaka nywele zao rangi kama anavyofanya staa wao na mhimili mkubwa wa timu, Pacome Zouzoua. Fundi wa mpira.

Wakati wakitinga robo fainali ya michuano hii mfumo ulikuwa tofauti na ulikuwa rahisi kidogo. Ukitinga tu makundi unakuwa umetinga robo fainali. Safari hii wametinga kwa staili ya aina yake huku wakimsaga Mwarabu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kiasi cha kocha kugombana wao na mchezaji wake katika benchi.

Deni la Yanga limekwisha na sasa bado deni la nchi. Saa 24 kabla Yanga haijafanya walichofanya Simba walikuwa wakihaha katika jiji la Abidjan kukabiliana na ASEC Mimosas. Pambano lilimalizika kwa suluhu, huku Sadio Kanoute alikosa nafasi ya wazi. Pengine leo tungekuwa tunazungumza lugha nyingine.

Suluhu hii inamuacha mnyama akiwa na kazi ndogo tu. Apate ushindi wa nyumbani dhidi ya Jwaneng Galaxy katika pambano la mwisho. Hata kama Waydad akishinda pambano la mwisho dhidi ya ASEC bado Simba atapita katika mfumo ule ule ambao umempitisha Yanga. Kwamba Mnyama atapita kwa sababu alimtwanga Wydad mabao mengi kuliko lile moja alilofungwa yeye kule Casablanca.

Sidhani kama Simba watafanya masikhara katika mechi hii. Wana sababu mbili za kutofanya masikhara. Kwanza ni kwamba watani tayari wamepita kwenda robo. Nchi itakuwa na matusi ya namna gani kwao kama wakishindwa kwenda robo fainali halafu kama hivi mtani wao kapita. Matusi yasiyomithilika.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement