Klabu za soka na wadau wa michezo wamehuzunishwa na taarifa za kifo cha aliyekuwa nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Ghana, Raphael Dwamena aliyefariki dunia baada ya kuanguka ghafla uwanjani wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Albania na kuzua gumzo mtandaoni.

Shirikisho la Soka la Albania lilithibitisha kifo cha Dwamena mwenye umri wa miaka 28 kutokana na mshtuko wa moyo wakati timu yake ya Egnatia ikicheza dhidi ya Partizani.

Picha kwenye mitandao ya kijamii zilimuonyesha mchezaji huyo akiwa peke yake na kuanguka dakika ya 24.

Taarifa rasmi kutoka timu ya taifa ya Ghana ilisema: "Chama cha Soka cha Ghana kinasikitika kusikia kifo cha mchezaji wetu wa zamani, Raphael Dwamena na kinapenda kutoa rambirambi zetu kwa familia yake katika wakati huu mgumu."

Hakuna maelezo juu ya sababu zilizotolewa na shirikisho la Albania lakini ripoti za vyombo vya habari vya ndani zilichunguza matatizo ya zamani ya moyo ambayo mchezaji huyo alikabiliwa nayo, ikiwa pamoja historia yake ya zamani wakati anakipiga Blau Veis Linz mwaka 2021 huko Austria kwani aliwahi kulazwa kutokana na matatizo ya moyo.

Kocha raia wa Brazil ambaye anaifundisha timu ya taifa ya Albania, Sylvinho, alisema kwenye mntandao wa kijami: "Pumzika kwa amani. Tunatoa pole na rambirambi kwa familia na marafiki"

"Mawazo yetu yako pamoja na familia yake na wapendwa wake katika nyakati hizi ngumu. Urithi wake katika klabu yetu utadumu milele," ilisema taarifa ya Levante

kwenye akaunti yao ya X. Zaragoza pia iliandika ujumbe wa pole kupitia akaunti ya X: "Tumesikitishwa na taarifa za kuondokewa na mchezaji wetu wa zamani Raphael Dwamena. Daima utabaki kwenye kumbukumbu ya mashabiki wa Zaragoza. Pumzika kwa amani"

Klabu za Hispania, Levante na Zaragoza zilituma rambirambi kutokana na kifo cha mchezaji wao zamani muda mfupi baada ya taarifa kutolewa. Dwamena alisajiliwa na Levante mwaka 2018 na alicheza msimu mmoja kabla ya kutolewa kwa mkopo Zaragoza msimu wa 2019-20.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement