GLASNER HAENDI POPOTE, ANANDAA MPANGO WA MUDA MREFU CRYSTAL PALACE
Kwa mujibu wa Sky Sports News (James Savundra & Kaveh Solhekol), Glasner anaendelea kudumisha uhusiano thabiti na uongozi wa Palace baada ya dirisha la usajili kumalizika kwa pilikapilika kubwa.
Ripoti zinasema kocha huyo wa Austria, aliyewahi kushinda Kombe la FA, amekuwa akihusiana na klabu katika mijadala ya malengo ya kati na ya muda mrefu, ingawa mustakabali wake binafsi bado haujakuwa wazi. Inadaiwa Glasner alikata tamaa na ukosefu wa uthubutu kwenye madirisha mawili ya usajili yaliyopita, lakini klabu imesisitiza kuwa haina wasiwasi kuhusu hali ya meneja.
Mapema mwezi huu, kulikuwa na madai kuwa Glasner alitishia kujiuzulu endapo nahodha Marc Guehi angebanduka kwenda Liverpool dakika za mwisho za dirisha. Hata hivyo, Glasner alikanusha uvumi huo na badala yake kumpongeza mwenyekiti Steve Parish kwa kuvunja makubaliano hayo bila mbadala sahihi kupatikana.
Baada ya mapumziko ya kimataifa, Glasner alisema:
“Kutakuwa na muda wa kuzungumza kuhusu mustakabali wangu.”
Palace sasa wanakabiliwa na mtihani mkubwa wikendi hii dhidi ya mabingwa watetezi Liverpool, huku wakiwa na nafasi ya kuifikia rekodi ya klabu ya kutokuwa na kichapo kwa mechi 18 mfululizo.



