TANZANIA MOJA YA MATAIFA 12 KUPELEKA TIMU NNE KIMATAIFA
Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika Soka Barani Afrika mara baada ya kuingia katika Orodha ya Shirikisho la Soka Barani Afrika kwa maana ya CAF, mataifa 12 yaliyopo nafasi ya juu Afrika.
Katika Orodha hiyo iliyotolewa na CAF inathibitisha kuwa Tanzania imekuwa moja ya Taifa kati ya Mataifa 12 ambayo yatapeleka timu nne kwenye michuano ya Kimataifa kwa maana ya Timu mbili Ligi ya Mabingwa Afrika na timu mbili Kombe la Shirikisho Afrika kwa msimu wa 2024/25
Mbali Na Tanzania, Nchi nyingine ni Algeria, Angola, Ivory Coast, Misri, Libya, Morocco, Nigeria, DR Congo, Afrika Kusini, Sudan na Tunisia.
Tukiendelea kuangazia kunako Michuano hiyo ya Kimataifa ya CAF
Msimu wa mashindano ya CAF Interclub 2024/25 kuanza kutimua vumbi kati ya Agosti 16 hadi 18 mwaka huu kwa raundi ya awali huku hatua za makundi zikipangwa kufanyika kati ya mwezi Oktoba hadi mwezi Desemba mwaka 2024.
Kwa upande wa Klabu za hapa nchini kwa maana ya Klabu ya Yanga itaanza kampeni zake za Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye raundi ya pili michuano hiyo na wataanzia ugenini huku Simba Sc ikianzia raundi ya pili ya kombe la Shirikisho Afrika nayo itaanzia ugenini.
Azam Fc itaanzia raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku Coastal Union wakianzia raundi ya kwanza ya kombe la Shirikisho Afrika.
Azam Fc na Coastal Union wataanzia nyumbani kwenye michuano hiyo ambayo inaanza kurindima kuanzia Agosti 16 mpaka 18.
Usajili wa wachezaji watakaoshiriki katika hatua ya awali utafanyika kati ya tarehe Julai 1, 2024 hadi Julai 20 huku Usajili wa wachezaji watakaoshiriki katika hatua ya pili ukitajwa kufanyika kati ya tarehe Julai 21 hadi Agosti 31 mwaka huu wa 2024.
Usajili wa wachezaji watakaoshiriki katika hatua ya makundi utafanyika kati ya Septemba 1 hadi Septemba 30, 2024.