TAIFA STARS YAANZA SAFARI YA MAANDALIZI YA MECHI YA KUWANIA KUFUZU KOMBE LA DUNIA DHIDI YA ZAMBIA
Mara baada ya kutamatisha ratiba ya mchezo wa kirafiki wa Kimataifa dhidi ya Timu ya Taifa ya Indonesia, Kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” chini ya Kocha Mkuu Hemed Morocco kimeanza safari ya kurejea nchini kwaajili ya maandalizi ya mchezo wa dhidi ya Zambia wa kuwania kufuzu kombe la Dunia.
“Kikosi cha Taifa Stars tayari kipo kwenye maandalizi kuelekea kwenye mchezo wa kufuzu Komb ela Dunia dhidi ya Zambia na kama ambavyo inafahamika kwamba Kocha ambaye anakaimu nafasi hiyo Kocha ambaye anakaimu nafasi hiyo kwamaana ya Hemed Suleiman maarufu kama Morocco tayari alikwakitaja kikosi na baadhi ya wachezaji walishaungana na kikosi na tulikuwa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Indonesia mchezo ambao tulimaliza kwa suluhu ya bila kufungana, ” Amesema Afisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo.
Ndimbo ameeleza kuwa mara baada ya kikosi cha Taifa Stars kuwasili kwaajili ya maandalizi ya mchezo huo utakaopigwa Ndola Nchini Zambia Juni 11 kitaendelea na maandalizi ambapo wachezaji ambao walikuwa katika majukumu yao katika Klabu za Azam na Yanga katika mchezo wa Fainali ya FA Tanzania Bara wameshaingia kambini jijini Dar es salaam wakiendelea na maandalizi huku wakiwasubiri wachezaji ambao wapo njiani kurejea Tanzania.
Ndimbo ameeleza kuwa katika kikosi hicho ni mchezaji mmoja mpaka sasa kutoka Azam FC Adolf Bitegeko akiwa ni ongezeko katika kikosi hicho.
Kwa upande wa hali za kiafya za wachezaji waliocheza mechi ya kirafiki dhidi ya Timu ya Taifa ya Indonesia, Ndimbo ameeleza kuwa mpaka sasa hakuna taarifa ya mchezaji ambaye amepata majeraha yatakayofanya ashindwe kucheza mchezo wa kuwania kufuzu kushiriki Kombe la Dunia dhidi ya Timu ya Taifa ya Zambia.
“Mpaka sasa bado hakuna taarifa ya kutisha ya kusema kwamba kunamchezaji pengine anaweza akakosa mchezo huo dhidi ya Zambia kwahiyo bado mpaka hivi sasa hali ya wachezaji ipo vizuri kuelekea kwenye mchezo wenyewe lakini kama unavyofahamu kwamba bado tunamuda wa kuelekea mpaka katika mchezo wenyewe kwahiyo hata kama kunamajeraha madogo madogo ambayo yatachukua siku mbili tatu maana yake ni kwamba bado muda upo, ” Amesema Afisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo.
Ndimbo ameongeza kuwa mara baada ya kikosi kuwasili kutakuwa na mazoezi kutokana na ratiba ya Kocha kabla ya kuanza safari kuelekea nchini Zambia.