Kiungo wa pembeni wa Yanga, Mahlatse Makudubela 'Skudu' amesema anachosubiri kwa sasa ni makocha wa timu hiyo kumpa nafasi kwenye timu na hiyo siku ikifika, atawaonyesha yeye ni nani.

Skudu aliyesajiliwa msimu huu kutoka Marumo Gallants ya Afrika Kusini, amerejea uwanjani hivi karibuni na kuwasha moto kwenye mechi tatu ikiwamo ya Kariakoo Derby baada ya kuumia kwenye mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam, alisema anachotaka ni kuaminiwa na kupewa muda wa kutosha ndani ya uwanja ili kuthibitisha usajili wake, akilenga mchezo ujao wa makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Yanga inatarajiwa kushuka uwanjani ikiwa ugenini Algeria kuvaana na CR Belouizdad Ijumaa ya wiki ijayo na Skudu aliliambia Mwanaspoti, kwa sasa yuko tayari kwa mapambano baada ya kupona majeraha.

"Niko fiti sana, ninachosubiri benchi la ufundi linipe muda wa kutosha uwanjani," alisema winga huyo. Kuhusu mchezo huo wa CR Belouizdad, Skudu alisema; “Nakiamini kikosi chetu na tupo tayari kwa mechi hii. Tuna timu iliyokamilika vizuri na tutakachojaribu kufanya ni kurudia mafanikio yetu ya msimu uliopita.

"Mwanzo mzuri umeonekana kwa mechi zetu za awali kwenye Ligi ya Mabingwa. Msimu uliopita tulicheza fainali Kombe la Shirikisho, malengo ni makubwa msimu huu."

Yanga imekuwa kwenye kiwango bora, ikishinda mechi nane kati ya tisa ilizocheza za Ligi Kuu Bara, ikipoteza moja dhidi ya Ihefu huku ikifunga mabao 26 na kufungwa matano na kuvuna jumla ya pointi 24, huku Skudu akicheza mechi tatu akitumia jumla ya dakika 76, zikiwamo 57 za Ihefu, dakika 18 za Singida Fountain Gate na dakika nne za mechi ya Simba na Yanga.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement