ROMANIA, UBELGIJI NA SLOVAKIA ZATINGA HATUA YA 16 BORA EURO 2024
Romania, Ubelgiji, na Slovakia zatinga katika 16 za mwisho huku Ukraine ikipoteza tiketi kutokana na tofauti ya magoli huku Kundi E Timu zote zikiwa na Pointi sawa.
Katika hali ambayo haijawahi kushuhudiwa, timu zote nne za Kundi E zilimaliza na pointi nne kila mmoja baada ya Ubelgiji na Ukraine kutoka sare ya bila kufungana mjini Stuttgart na Romania na Slovakia kutoka sare ya bao 1-1 mjini Frankfurt.
Ubelgiji kwa kipindi kirefu haikuridhisha kwa mara nyingine na ililazimika kuwa makini kwa sababu ushindi kwa Ukraine ungewaondoa mashindanoni.
Matokeo hayo sasa yana maana kuwa Ubelgiji yake Kevin De Bryune itakuwa na kibarua kikali dhidi ya Ufaransa yake Kylian Mbappe Jumatatu jioni huku Wapinzani wa Slovakia watakuwa ni England siku ya Jumapili jioni.
Georgia wanashiriki mashindano makubwa ya kandanda kwa mara ya kwanza tangu Uhuru ambapo iliiduwaza Ureno na kutinga hatua ya mtoano, kwa mara yao ya kwanza kabisa katika mashindano makubwa baada ya kuwafunga mabingwa hao wa zamani wa Ulaya bao 2-0. Ureno ambao walikuwa tayari wamefuzu, walifanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi cha kwanza.
Ushindi huo wa kushangaza wa Georgia unawapa zawadi ya kukutana na Uhispania Jumapili usiku na una maana walifuzu kama moja ya timu nne bora zilizomaliza katika nafasi ya tatu kwenye makundi, Pamoja na Slovenia, Uholanzi na Slovakia.
Uturuki pia ilijiunga nao baada ya kuwatimua Waczech kwa kuwafunga bao2-1 huku Hungary hatimaye wakikubali hatima yao.