NYOTA WA KIMATAIFA MBWANA SAMATTA HAJAJUMUISHWA KATIKA KIKOSI CHA TIMU YA TAIFA KINACHOJIANDAA NA MCHEZO WA KUFUZU KOMBE LA DUNIA
Kaimu Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya wanaume, Hemed Suleiman ‘Morocco’ hajamjumuisha Nahodha, Mbwana Ally Samatta sambamba na Beki wa Klabu ya Yanga Dickson Job katika kikosi cha wachezaji 34 cha Taifa Stars kitakachoingia kambini kujiandaa na mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Zambia.
Tanzania imepangwa pamoja na Morocco, Zambia, Niger, Kongo na Eritrea ambayo imejitoa katika Kundi E kufuzu Kombe la Dunia 2026 zinazoandaliwa kwa pamoja na Canada, Mexico na Marekani.
Taifa Stars ilianza vyema kampeni zake za Kombe la Dunia 2026 kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Niger Novemba 18 mwaka jana Uwanja wa Marrakech nchini Morocco, bao pekee la mshambuliaji mzaliwa wa DRC, Kokola Charles William M'Mombwa wa Macarthur FC ya Australia.
Taifa Stars inatarajiwa kushuka Uwanja wa Levy Mwanawasa Jijini Ndola kumenyana na Zambia katika mchezo wake wa pili wa kufuzu Kombe la Dunia.
Kwa upande wa Timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars, kimeendelea na mazoezi kwaajili ya maandalizi ya mechi ya kirafiki dhidi ya Timu ya Taifa ya Mali na Sudan huku Kocha wa Kikosi hicho Bakari Shime akiwa amemjumuisha mshambuliaji wa Al Nasr ya Saudi Arabia Clara Luvanga katika kikosi cha wachezaji 22 cha timu hiyo.