MICHUANO YA SOKA LA UFUKWENI TANZANIA YAPOTEZA KWA KUCHAPWA GOLI 5-4 DHIDI YA MOZAMBIQUE
Michuano ya Soka la Ufukweni ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu kusini mwa Afrika maarufu kama COSAFA BEACH SOCCER imeendelea kutimua vumbi nchini Afrika kusini huku Timu ya Taifa ya Tanzania ya Soka la ufukweni ikiendelea kubeba matokeo mabaya kunako michuano hiyo mara baada ya kupoteza kwa bao 5-4 dhidi ya timu ya Taifa ya Mozambique.
Katika mchezo wa awali Tanzania ilianza vibaya kwa kupoteza kwa bao 3-2 dhidi ya Timu ya Taifa ya Angola ambapo kwa sasa imebakiza mchezo mmoja pekee wa hatua ya makundi dhidi ya Morocco utakaopigwa Machi 20 South Beach Arena, Durban nchini Afrika Kusini
Nahodha wa Kikosi hicho, Jaruph Juma ameeleza wazi kuwa licha ya upoteza mchezo huo lakini wameridhishwa na hali ya upambanaji wa kikosi.
“Kiujumla matokeo hatujayapokea vizuri lakini mimi binafsi pamoja na wachezaji wenzangu tumeridhishwa na kiwango ambacho tumekionyesha tofauti na mechi iliyopita, hii yote ni katika muendelezo wa kujaribu kutenngeneza timu, “
“Mwalimu kunawachezaji amewapa nafasi ambao ni wachezaji wapya kwenye Beach Soccer amewatambulisha kwenye mchezo huu na kwenye haya mashindano, yote ni katika kuendeleza kuboresha hii timu ili kuona kwamba tunaenda kufanya vizuri kwenye mashindano makubwa ya Mataifa ya Afrika, “
Jaruph amewataka watanzania kuendelea kuwasapoti kwani bado wapo kwenye jitihada za kutoa mchango kwa Taifa kama wachezaji pamoja na benchi la Ufundi.
Michuano hiyo iliyoanza kutimua vumbi March 17, itatamatika March 23 Mwaka huu kwa mchezo wa Fainali huku Michuano hiyo ikiwa imegawanywa katika makundi mawili, Tanzania ipo Kundi B ikiwa na timu kutoka Mataifa ya Morocco, Mozambique na Angola huku Kundi A likiwa limebeba timu kutoka Mataifa ya Malawi, Saudi Arabia, Seyshelles na Mwenyeji Afrika Kusini.