Hispania kuvaana na Ufaransa kwenye mechi ya nusu fainali katika michuano ya Euro 2024 baada ya kufanikiwa kuwabwaga wenyeji, Ujerumani, mabao mawili kwa moja katika mchezo wa usiku wa kuamkia leo.


Dani Olmo ndiye aliyepachika goli la kwanza la Uhispania katika dakika ya 51, ambalo lilirejeshwa na Florian Witz wa Ujerumani katika dakika ya 89, kabla ya Mikel Merino kuandika ushindi kwa mkwaju wa dakika za nyongeza.

Merino mwenye umri wa miaka 28 alishangiria kwa kuigiza staili ya baba yake, Miguel Merino. Aliwaambia waandishi wa habari kwamba goli lake ni alama ya kihistoria kwenye uwanja wa Stuttgart, ambako zaidi ya miongo mitatu iliyopita, baba yake alipachika goli la ushindi kwa timu yake ya Osasuna dhidi ya Sttutgart Novemba 1991.

Kwa upande mwengine, mechi kati ya Ureno na Ufaransa ilimalizikia kwa mikwaju ya penalti baada ya dakika za kawaida na za nyongeza kumalizika bila timu yoyote kuliona lango la mwenzake. 

Mkongwe wa soka la kulipwa, Cristiano Ronaldo alitoka uwanjani bila kuipatia Ureno goli lolote lile, ikiwa ni mara ya kwanza kwenye historia yake ya soka. 

Kocha wa Ufaransa, Didier Dechamps, amesema ushindi wao ulipatikana kwa tabu kwa kuwa wamecheza na mojawapo wa timu bora kwenye kandanda ya Ulaya. 

Ronaldo (39) amecheza Euro yake ya mwisho 2024 akihitimisha mechi 212 katika mashindano yote, amefanikiwa kufunga mabao 130 pamoja na kutoa asisti 36 huku akiwa ameshinda mataji mawili katika timu ya taifa kwa muda wote aliocheza.

Naye Kepler Laveran de Lima Ferreira “Pepe” (41) ambaye itakuwa ni Euro yake ya mwisho ameichezea Ureno mechi 140 katika mashindano yote na kufanikiwa kufunga mabao 8 pamoja na kushinda mataji mawili.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement