FAINALI YA COPA AMERICA 2024 ARGENTINA DHIDI YA COLOMBIA
Timu ya taifa ya Colombia imeifuata Argentina kwenye fainali ya kombe la Mataifa ya Amerika Kusini Copa America 2024 kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya Uruguay licha ya kumaliza mchezo pungufu ya mchezaji mmoja baada ya beki wa Crystal Palace, Daniel Munoz kuoneshwa kadi nyekundu mwishoni mwa kipindi cha kwanza.
Kiungo wa zamani wa Real Madrid, James Rodriguez ameendelea kujiweka katika nafasi nzuri ya kumaliza kama mchezaji bora wa mashindano akiandika asisti yake ya 6 kwenye michuano hiyo baada ya kumtengea Jefferson Lerma wa Crystal Palace na kuandika bao la ushindi kwa Colombia.
Colombia almaarufu ‘Los Cafeteros’ wanaelekea fainali huku wakiendeleza rekodi yao ya kutopoteza kwenye mechi 28 mfululizo (ushindi mara 22 na sare 6) lakini watakuwa na kibarua kigumu dhidi ya bingwa mtetezi, Argentina kwenye fainali itakayopigwa alfajiri ya Julai 15, 2024.
FT: Uruguay 0-1 Colombia
⚽ Lerma 39’ (🅰️ James Rodriguez)
Baada ya kuchezea kichapo cha 1-0 dhidi ya Colombia, Uruguay watakabiliana na Canada iliyochapwa 2-0 na bingwa mtetezi, Argentina kwenye kuwania nafasi ya mshindi wa tatu alfajiri ya Julai 14, 2024.