ELIUD KIPCHOGE AUNGA MKONO UGANDA KUCHUKUA UBINGWA KABLA YA KUANZA KWA MARATHON
Joshua Cheptegei bado hajawahi kukimbia marathon lakini bingwa mara mbili wa Olimpiki Eliud Kipchoge anaamini kuwa Mganda huyo anaweza kuwa mwanariadha mwenye kasi zaidi duniani kwa zaidi ya maili 26.2.
Cheptegei alishinda medali ya dhahabu ya mita 5,000 katika Michezo ya Tokyo 2020 na anashikilia rekodi ya ulimwengu kwa umbali huo na mita 10,000.
Kipchoge, ambaye ndiye anayempa hamasa, sasa anamuunga mkono Cheptegei kabla ya mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 27 kuanza kukimbia mbio za marathon kwa mara ya kwanza mjini Valencia Jumapili.
"Tayari anashikilia rekodi katika nyanja zingine na ana nafasi kubwa ya kuvunja rekodi ya ulimwengu katika mbio za marathon," Kipchoge aliambia BBC Sport Africa."Joshua ana kipaji na nidhamu. Pia anajifunza vyema.
"Nina furaha Joshua anajaribu kitu kipya. Nitakuwa nikitazama na kumpa motisha kama kawaida."
Cheptegei anachukuliwa kuwa mmoja wa wakimbiaji bora zaidi wa mbio za masafa marefu duniani, akiwa na mataji matatu ya dunia ya mita 10,000 na taji la dunia la mbio za nyika pamoja na dhahabu ya Olimpiki.
Hapo awali alishikilia rekodi za dunia za mbio za kilomita 5 na 10 na akafunzwa na Kipchoge, ambaye alivunja rekodi ya marathon mara mbili, mnamo 2015 huko Kaptagat.
Mkenya huyo anasema "ukuaji" wa Cheptegei umetokana na umbali mbalimbali wa mbio alizokimbia, lakini kijana huyo mwenye umri wa miaka 39 amemshauri raia huyo wa Uganda kukimbia mbio zake binafsi siku ya Jumapili.
"Kipchoge alinitia moyo sana nilipokuwa nikianza taaluma yangu, urithi wake unanitia moyo," Cheptegei alisema.
Maneno yake ya ukarimu siku zote yameweza kuniongoza kwa siku na miaka. Eliud huwa ananifuatilia, anatuongoza katika njia nzuri.
"Ni heshima kubwa kujifunza kutoka kwa wakuu. Kwa heshima hii maalum, ninatazamia kutumia kile tunachoshirikishana pamoja kila wakati."