Baba wa mzaliwa wa Colombia anayeichezea Liverpool Luis Díaz ameachiliwa na waasi wa mrengo wa kushoto ambao walimteka nyara siku 13 zilizopita, vyanzo vya polisi na vyombo vya habari vya ndani vinasema.

Luis Manuel Díaz alikabidhiwa kwa maafisa wa Umoja wa Mataifa na wa Kanisa Katoliki na wanachama wa Jeshi la Ukombozi wa Kitaifa (ELN).

Alitekwa nyara tarehe 28 Oktoba katika mji wa nyumbani wa familia hiyo, Barrancas Mama wa mwanasoka huyo pia alikamatwa, lakini aliachiliwa ndani ya saa chache.

Vyombo vya habari vya eneo hilo vilisema Bw Díaz alikuwa amesafiri kwa helikopta ya kijeshi hadi jiji la Valledupar, ambapo alifanyiwa uchunguzi wa kimatibabu kabla ya kurejeshwa kwa familia yake.

Pia walinukuu mamlaka zikisema kwamba alikuwa katika hali nzuri ya afya, bila dalili za kuumizwa.

Kulingana na gazeti la El Tiempo, kulikuwa na matukio ya vilio katika mtaa walipokuwa wakiishi wanandoa hao, huku wanafamilia wakipakia magari yao barabarani kusherehekea.

Wengi wao walikuwa wamevalia jezi za timu ya Liverpool zenye nambari 23 na jina la Luis Díaz.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement