Simba na Yanga kwa nyakati tofauti wamenasa saini za wachezaji wa JKU inayoshiriki Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), lakini kocha wa timu hiyo, Salum Ali Haji amewataka viongozi wa timu hizo kuwa na subira na wachezaji hao.

Yanga ndio ilianza kunasa saini ya kiungo mshambuliaji, Shekhan Ibrahim Khamis (18) na baadaye watani wao Simba wakamsaini Saleh Karabaka (23) ambaye pia anacheza nafasi hiyo. Karabaka ameanza na mguu mzuri ndani ya Simba baada ya kufunga bao kwenye mechi ya kwanza ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanayoendelea Uwanja wa New Amaan Complex, kisiwani Unguja katika ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya JKU mabaye ni timu yake ya zamani.

Kocha huyo aliwachambua wachezaji hao kwa nafasi zao ndani ya timu mpya kuwa kitu cha kwanza ni uwepo wa subira pande zote mbili, mchezaji na viongozi wa timu likiwemo benchi la ufundi.

Haji alisema wachezaji wote hao ambao walikuwa kwenye kikosi cha kwanza cha timu yake ni wazuri lakini sio kwa mahitaji ya mafanikio ya haraka.

"JKU ni kituo cha kulea na kukuza vijana, Shekhan amelelewa hapa JKU Academy tangu akiwa na miaka 11 hadi anaenda Yanga, ni mchezaji mzuri ila kama hapa alikuwa staa basi asitarajie hilo ndani ya Yanga kwa muda mfupi.

"Ili aje kuwa bora zaidi basi anaweza kuchukua muda wa misimu miwili ila atawasaidia kutokana na umri wake mdogo. "Kwa upande wa Karabaka ni mchezaji mzuri, ana kasi na anajua kupiga mipira kama Simba wanavyocheza lakini naye sio wa kuwapa mafanikio wanayoyataka sasa hivi.

"Wachezaji wanatakiwa kujituma, miaka ya hivi karibuni wamekosa uvumilivu pale wanapokosa nafasi ya kucheza ingawa ukiangalia timu kama Yanga na Azam huwa zinadumu nao sana ukilinganisha na Simba, hii huenda inatokana na mifumo yao" alisema Haji.

Kocha huyo alisema walimsajili Karabaka kutoka timu ya Hard Rock ya Pemba ambao walimsajili akitokea timu moja inayoshiriki ligi za daraja la chini huko Tanga.

"Karabaka hajalelewa kwenye akademi yetu na hajapita kwenye mfumo huo, hapa kwetu amekaa misimu miwili akitokea Hard Rock ambao pia walimsajili kutoka mkoani Tanga, hivyo kuna tofauti hata kwenye umri wao."

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement