ZAMALEK YATWAA UBINGWA WA KOMBE LA SHIRIKISHO BARANI AFRIKA
Bao la dakika ya 23 ya mchezo lililopachikwa na Ahmed Hamdi limetosha kuiwezesha Zamalek ya Misri, kutwaa taji la Kombe la Shirikisho Afrika mbele ya RS Berkane.
Katika mchezo huo Zamalek waliokuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Cairo, waliingia uwanjani kusaka ushindi baada ya mchezo wa awali kuchapwa mabao 2-1. Ushindi huo umewafanya kuibuka mabingwa wapya kwa faida ya bao la ugenini.
Winga wa zamani wa Yanga, Tuisila Kisinda aliyeingia kipindi cha pili kuongeza nguvu hakuweza kuwakomboa wababe hao wa Morocco dhidi ya kipigo hicho kilichofuta ndoto ya kubeba taji hilo la pili kwa ukubwa barani Afrika, nyuma ya lile la Ligi ya Mabingwa.