Mshambuliaji wa KMC, Wazir Junior ameonyesha umwamba wake baada ya kutupia ‘hat trick’ timu yake ilipoichapa Tabora United mabao 4-2, kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Hii ni hat trick ya tano kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, baada ya nyingine za awali kufungwa na Feisal Salum 'Fei Toto' wa Azam, Jean Baleke akiwa na Simba, Stephen Aziz Ki Yanga na Kipre Junior Azam.

Hata hivyo, Tabora imeweka rekodi ya wachezaji wawili kufunga ‘hat trick’ dhidi yake baada ya awali Fei Toto kufanya hivyo kwenye mchezo wa kwanza kabisa wa Ligi Kuu.

Junior alitumia dakika 20 tu kufunga hat trick yake ya kwanza msimu huu baada ya kufunga katika dakika za 49, 60 na 67 na kuwa mzawa wa pili aliyefunga idadi hiyo ya mabao kwenye mchezo mmoja wa ligi msimu huu.

Sasa staa huyo amesogea hadi nafasi ya pili kwenye chati ya ufungaji akifunga mabao 11 sawa na Aziz Ki, lakini akiwa bao moja nyuma ya kinara wa mabao kwa sasa, Fei Toto mwenye 12.

KMC imesogea hadi nafasi ya nne kwenye msimamo ikiwa na pointi 28 moja mbele ya Coastal Union yenye 27, huku Tabora ikibaki kwenye nafasi ya 13 na pointi 21.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement