Mamia ya Vijana na watoto wenye vipaji vya kukimbiza na kucheza na Pikipiki maarufu kama Dede, wameanza kujifua kwenye viwanja vya Magereza Jijini Arusha ikiwa ni maandalizi ya msimu mkubwa wa mashindano ya Pikipiki yanayosimamiwa na kuratibiwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda.

Kufanyika kwa mashindano hayo baadae mwezi Julai mwaka huu ni utekelezaji wa vitendo wa maelekezo ya Mhe. Mkuu wa Mkoa ya kuwataka watendaji wote wa Mkoa wa Arusha kutumia nafasi zao kuhakikisha kando na mengine, wanalea, kustawisha na kuwa sababu ya kukuza na kuimarisha vipaji, Biashara na kazi za mikono ya wakazi wote wa mkoa wa Arusha.. 

Mhe. Paul Christian Makonda ametangaza kufanyika kwa mashindano hayo ya pikipiki kila mwaka kwa kushirikisha waendesha pikipiki kutoka ndani na nje ya Tanzania ambapo Mshindi wa kwanza ataondoka na Milioni kumi za Kitanzania kando ya zawadi nyingine mbalimbali.

Baadhi ya washiriki wa maandalizi hayo wamemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwa kutambua na kuwekeza nguvu zake katika mchezo huo pamoja na kwenye kukuza vipaji vya wana Arusha huku pia wakimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uteuzi wa Mhe.Makonda ambaye amedhihirisha namna anavyojali na kuthamini vipaji na makundi mbalimbali kwenye jamii.

Kutamatika kwa mashindano hayo kutafungua msimu mwingine wa mashindano ya kimataifa ya magari aina ya Land Rover pekee ambayo kulingana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, mashindano hayo yatafanyika mwishoni mwa mwaka huu ikiwa ni sehemu ya kuwa na michezo na shughuli mbalimbali zitakazovutia wageni na watalii wanaofika mkoani Arusha, suala ambalo litasisimua na kukuza uchumi wa Arusha na kuongeza matumizi ya fedha kutoka kwa wageni wanaofika Arusha.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement