WAJUMBE 19 WA KAMATI MAALUMU YA HAMASA YA TIMU ZA TAIFA
Dar es Salaam. Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro ameteua wajumbe 19 wa kamati maalumu ya hamasa ya timu za Taifa zilizofuzu mashindano mbalimbali ya kimataifa.
Tanzania imefuzu kushiriki Fainali za Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON nchini Ivory Coast, michuano hii inaanza Januari 13 - Februari 11, 2024. Pia, Tanzania 'Twiga Stars' imefuzu kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (WAFCON).
Kamati hiyo iliyotangazwa jana Jumatano Januari, 2024 kupitia taarifa iliyotolewa na Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Mwenyekiti ni Theobald Thabi, Makamu Mwenyekiti, Patrick Kahemela na katibu ni Neema Msitha.
Wajumbe ni Beatrice Singano, Michael Nchimbi, Jemedari Said, Nick Reynolds (Bongozozo), Hamis Ally, Christina Mosha, Rais wa Yanga, Mhandisi Hersi Said na Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Salum Abdallah Try-again. Pia, yumo Paulo Makanza, Mohamed Soloka, Hassan Mohamed Raza, Lucas Mhavile Joti, Oscar Oscar, Prisca Kishamba na Burton Mwemba (Mwijaku) na Clyaton Chipondo (baba levo).
"Kamati hii itakuwa na jukumu la kuhamasisha mashabiki na wapenzi wa michezo ndani na nje ya nchi kujitokeza kushangilia na kuziunga mkono timu za Taifa na kuratibu hafla maalumu ya harambee ya kuzichangia timu za Taifa itakayotarajiwa kufanyika Januari 10, 2024 Dar es Salaam," inaeleza taarifa hiyo.
Hafla hiyo itakayofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Johari Rotana, Dar es Salaam Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atamuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.