MFUNGAJI Bora wa Ligi Kuu Bara, Safari imezidi kupamba moto kwa viungo washambuliaji kufuatia nyota wa Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto' usiku huu kujibu mapigo kwa fundi wa Yanga, Stephane Aziz Ki.

Fei Toto amefunga bao pekee lililoipa Azam ushindi wa 1-0 dhidi ya Ihefu katika pambano kali la Ligi Kuu lililopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex na kuifanya timu hiyo kufikidha pointi 54 baada ya mechi 24 na kuganda nafasi ya pili nyuma ya Yanga yenye 58 kwa mechi 22.

Bao hilo lililofungwa katika dakika ya 13 ya mchezo huo linakuwa la 14 kwa Fei Toto, moja pungufu aliyonayo Aziz Ki mwenye 15 akiongoza orodha ya wafungaji wa ligi hiyo.

Aziz Ki alifunga bao la 15 katika Kariakoo Dabi wakati Yanga ikiizamisha Simba kwa mabao 2-1.

Fei toto ameonekana kuwa mwiba katika mchezo huo kutokana na uhuru aliokuwa nao, huku akitumika nyuma ya Kipre Jr aliyecheza kwa dakika 85 kama mshambuliaji wa mwisho.

Kwa matokeo hayo Azam imepunguza pengo la pointi baina yao na Yanga kutoka saba hadi nne, licha ya kuwa na mechi mbili zaidi dhidi ya watetezi hao wa ligi.

Pia Azam imeongeza pengo la pointi baina yao na Simba iliyopo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 46 kutoka kuwa tano hadi nane, japo imekuwa mbele kwa michezo mitatu tofauti na Simba yenye michezo 21.






You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement