BODI ya Ligi Kuu Tanzania imesitisha matumizi ya uwanja wa Jamhuri uliopo mjini Morogoro kwa michezo ya Ligi Kuu ya NBC kutokana na mapungufu kadhaa kwenye miundombinu ya uwanja inayosaidia urushaji wa matangazo mbashara ya runinga.

Uamuzi wa kusitisha matumizi ya uwanja huo umekuja baada ya mdhamini mwenye haki za matangazo ya runinga, Azam Media Limited, kuieleza Bodi ya Ligi Kuu kuhusu changamoto walizoendelea kukutana nazo katika maandalizi ya urushaji matangazo mbashara ya michezo ya Ligi Kuu ya NBC, hata baada ya kufanya jitihada mbalimbali za kuboresha miundombinu hiyo.



Klabu ya Simba ambayo ilikuwa ikiutumia uwanja huo kwa michezo yake ya nyumbani, ilishiriki kikamilifu katika majadiliano yaliyozaa maamuzi ya kusitisha matumizi ya uwanja huo na kwamba klabu hiyo sasa itatumia uwanja wa Azam Complex uliopo Dar es Salaam kwa michezo yake ya nyumbani.

Hata hivyo, uwanja wa Jamhuri utaendelea kutumika kwa michezo ya mashindano mengine yote yaliyo chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania ikiwemo Ligi ya Championship ya NBC na First League zinazoendeshwa na kusimamiwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement