MECHI ya Yanga na KMC inayotarajia kupigwa Jumamosi ijayo, itachezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro huku Simba kuhusishwa kuutumia uwanja huo kwenye mechi za nyumbani.

Yanga inaenda Jamhuri ikiwa na mastaa kama Pacôme Zouzoua, Aziz Ki, Max Nzengeli, Yao na Simba itawakilishwa na Clatous Chama, Saido Ntibazonkiza, Pa Job, Freddy na Babacar Sarr.

Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Mwakasungula alithibitisha hilo kama wenyeji wa mchezo huo, wanakwenda kuchezea Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

"Mchezo wetu tunakwenda kuchezea Jamhuri, hivyo mashabiki wetu tunaomba wajiandae kwenda huko kuisapoti timu yetu,"amesema.

Wakati huo huo, habari za ndani kutoka Simba zinasema uwanja wa mechi zao za nyumbani watautumia wa Jamhuri, Morogoro.

"Baada ya kumaliza mechi za Kanda ya Ziwa, tutautumia Uwanja wa Jamhuri, Morogoro kuchezea mechi za nyumbani," kilisema chanzo hicho.

Simba na Yanga zilikuwa zinatumia Uwanja wa Benjamin Mkapa na Uhuru kwa mechi za nyumbani, lakini baada ya viwanja hivyo kufungwa kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati zililazimika kutafuta sehemu nyingine kwa ajili ya michezo ya Ligi Kuu.

Japokuwa Yanga haijathibitisha kwamba Uwanja Azam Complex ndio utatumika kwa mechi zake za nyumbani, lakini imekuwa ikiutumia kuchezea.

Kwa upande wa Simba, inaelezwa tayari imewasilisha barua katika Bodi ya Ligi ili kuanza kuutumia Jamhuri kwa mechi za nyumbani.

Hata hivyo, kwa mechi za Ligi ya Mabingwa inayotarajiwa kurejea wiki mbili zijazo, timu hizo mbili zinatarajiwa kutumia Uwanja wa Mkapa, baada ya serikali kuzikubalia kuutumia kwa ajili ya mechi za kimataifa pekee.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement