USM ALGER YAGOMA KUINGIZA TIMU UWANJANI MCHEZO WA NUSU FAINALI YA PILI KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA
Bingwa mtetezi wa Kombe la Shirikisho Afrika, USM Alger ya Algeria imegoma kuingiza timu kwenye Uwanja wa Berkane Municipal kwa ajili ya mchezo wa nusu fainali ya pili ya michuano hiyo dhidi ya RS Berkane ya Morocco, uliopangwa kupigwa saa 4:00 usiku.
USM Alger ilifika hadi kwenye vyumba vya kubadilishia nguo lakini hawakuingia uwanjani na badala yake wameondoka na kuwaacha wenyeji Berkane.
mchezo wa nusu fainali ya kwanza ulishindwa kufanyika baada ya wageni Berkane kuzikataa jezi walizozikuta kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wakidai sio zao.
Awali, RS Berkane ilidai jezi zao zilizuiwa Uwanja wa Ndege walipowasili Algeria kisha wakawaambia hawataruhusiwa kuzitumia kwa kuwa zina Bendera ya Morocco, jambo lililopingwa na timu hiyo, wakidai wanataka kuzitumia na ikishindikana hawataingiza timu uwanjani, jambo ambalo lilitokea.
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilifanya uamuzi wa kuipa ushindi RS Berkane wa alama tatu na mabao 3-0 baada ya kubaini Wamorocco hao walifanyiwa vitendo visivyo vya kiungwana na wenyeji wao USM Alger.
Wadau wanasubiri maamuzi kutoka Caf kwa kuwa kidiplomasia nchi hizo mbili hazina uhusiano mzuri ikitajwa chanzo cha USM Alger kukataa kuingiza timu uwanjani.