TIMU ya Simba imetinga kibabe hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 6-0, dhidi ya TRA ya Kilimanjaro katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamanzi.

Katika mchezo huo wa hatua ya 32 bora, shujaa wa Simba ni kiungo wa kikosi hicho, Sadio Kanoute aliyefunga mabao matatu 'hat-trick' huku mengine yakifungwa na Ladaki Chasambi, Pa Omar Jobe na Freddy Michael waliofunga moja kila mmoja wao.

Ushindi huo kwa Simba ni salamu tosha kwa wapinzani wao Jwaneng Galaxy watakaokutana nao Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam katika hatua ya makundi kuwania tiketi ya kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba iliyokuwa kundi 'B' la michuano hiyo inahitaji ushindi kwenye mchezo huo ili kukata tiketi ya kufuzu hatua ya robo fainali kwani itafikisha pointi tisa na kushika nafasi ya pili nyuma ya vinara ASEC Mimosas iliyofuzu na pointi 11.

Kikosi hicho chenye pointi sita sawa na Wydad Casablanca ya Morocco, endapo kitashinda mchezo huo kitafuzu moja kwa moja bila ya kujali matokeo ya mchezo mwingine wa kundi hilo utakaopigwa kati ya Wydad itakayoikaribisha ASEC Mimosas.

Hadi sasa tayari timu sita zimeshafuzu robo fainali ambazo ni ASEC Mimosas (Ivory Coast), Yanga (Tanzania), Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), Al Ahly (Misri), Petro de Luanda (Angola) na TP Mazembe kutoka nchi ya Kidemokrasia ya Congo.

You Might Also Like

Get Newsletter

Advertisement