USHINDI WA KOMBE LA FA BADO HAUTOSHI KULINDA KIBARUA CHA KOCHA WA MANCHESTER UNITED ERIK TEN HAG
Erik ten Hag ni kocha bora kabisa wa Manchester United tangu Sir Alex Ferguson alipong'atuka, lakini namba zake bado hazitoshi kukifanya kibarua chake kuwa salama.
Kocha huyo Mdachi anaweza kufutwa kazi licha ya kushinda Kombe la FA baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Manchester City kwenye fainali iliyofanyika Wembley, Jumamosi iliyopita.
Ten Hag, 54, ameiongoza Man United kwenye mechi 114 tangu alipoteuliwa mwaka 2022. Katika msimu wake wa kwanza, aliongoza timu kuwamo Top Four Ligi Kuu England na kushinda Kombe la Ligi. Msimu wa pili mambo yametibuka, timu imemaliza nafasi ya nane kwenye ligi, lakini imefanikiwa kushinda ubingwa wa Kombe la FA.
Shida inayomkabili ni klabu ipo chini ya tajiri Sir Jim Ratcliffe, ambaye anahitaji mafanikio na hilo ndilo linalotishia usalama wa kibarua cha kocha huyo wa zamani wa Ajax.
Kwa msimu uliomalizika, Man United ilifanya vibaya pia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na ilimaliza ya mwisho kwenye kundi lake, hivyo kukomea hatua hiyo ya makundi.
Kwa jumla, Ten Hag ameshuhudia ushindi kwenye mechi 66 katika muda wake aliokuwa na miamba hiyo ya Old Trafford, hivyo akiwa na wastani wa ushindi wa asilimia 57.9.
Hata hivyo, hiyo ni rekodi bora kabisa kuzidi makocha wengi waliokuja kuinoa Man United baada ya Ferguson. Ten Hag amekuwa na rekodi bora kuwazidi Ralf Rangnick, Ole Gunnar Solskjaer, Louis van Gaal na David Moyes na amezidiwa na Jose Mourinho pekee.
Rangnick ndiye mwenye wastani mdogo zaidi wa ushindi, akiwa na asilimia 38 tu katika mechi zake 29, wakati Solskjaer ana wastani wa asilimia 54.2 na Mourinho ana asilimia 58.3.
Van Gaal ana asilimia 52.4 ya ushindi mbaya kuzidi David Moyes mwenye asilimia 52.9.
Ten Hag amepoteza mechi nyingi kuzidi makocha wengine wote, isipukuwa mmoja, Solskjaer.
Ten Hag amepoteza mechi 31, wakati Solskjaer amepoteza mechi 40 kwenye 168.
Kwa makocha hao, Mourinho ndiye aliyefanikiwa zaidi, akibeba Kombe la Ligi, Europa League na Ngao ya Jamii kwa muda wake aliokuwa na kikosi hicho cha Old Trafford.