UMUHIMU WA POINTI TATU LEO TABORA UNITED DHIDI YA SIMBA
DAKIKA 90 za mchezo wa leo kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora zina maana kubwa kwa kila timu wakati Tabora United itakapoialika Simba kuanzia saa 10:00 jioni.
Umuhimu wa pointi tatu ambazo zitafanya kila timu ijiweke katika nafasi nzuri kwenye msimamno wa ligi unachangia kwa kiasi kikubwa kuifanya mechi hiyo kuwa ya kipekee kwa pande hizo.
Kwa mwenyeji Tabora United, matokeo ya ushindi yataifanya isogee hadi nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi kwani itafikisha pointi 18 na hivyo kutoka katika nafasi ya 12, iliyopo sasa.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Tabora United, Simba yenyewe inahitaji ushindi ili iendelee kukimbizana kwa ukaribu na Yanga na Azam FC katika mbio za ubingwa ambapo ikishinda itafikisha pointi 29 na kuzidi kujishindilia katika nafasi ya tatu inayoishikilia.
Simba ina kumbukumbu nzuri na Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ambao utachezewa mechi hiyo kwani mara ya mwisho kucheza hapo ilikuwa ni dhidi ya KMC, Desemba 24, 2021 ambapo iliibuka na ushindi wa mabao 4-1.
Timu mwenyeji inaikaribisha Simba ikiwa imetoka kufanya vibaya kwenye mechi zake tatu mfululizo za Ligi Kuu ambazo imetoka sare moja na kupoteza michezo miwili.
Tabora United wamekuwa na mwendelezo wa kufanya vizuri katika mechi za nyumbani kama ilivyo kwa Simba kwenye mechi za ugenini msimu huu na uthibitisho ni mechi tano zilizopita kwa timu hizo ambapo zimevuna idadi kubwa ya pointi kuliko zilizopoteza.
Katika mechi tano zilizopita ambazo Tabora United imecheza nyumbani, imekusanya pointi 10, ikipata ushindi mara tatu, sare moja na kupoteza mchezo mmoja wakati Simba imekusanya pointi 13 katika mechi tano zilizopita ilipokuwa ugenini, ikishinda nne na kutoka sare moja.
Ni mchezo ambao unakutanisha makocha wawili waliowahi kufanya kazi pamoja ambao ni kocha mkuu wa Tabora United, Goran Kopunovic na msaidizi wa Simba, Selemani Matola ambao walikuwa mtu na msaidizi wake ndani ya kikosi cha Simba mwaka 2015.
Hii ni mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana sio tu kwenye Ligi Kuu bali pia hata katika mashindano mengine na hivyo mshindi ataandika historia ya kuwa wa kwanza kushinda baina yao, Kocha msaidizi wa Simba Seleman Matola alisema wapo tayari kukabilianana Tabora United leo.
"Unapocheza na timu kama Tabora mechi inakuwa ngumu. Tumekuja tukiwa tumejiandaa, tuko vizuri pamoja na ugumu ambao watakuwa nao sababuni muhimu kupata pointi tatu," alisema Matola.
Kocha wa Tabora United, Goran Kopunovic alisema kuwa licha ya kuwaheshimu Simba, wamejipanga kuhakikisha wanapata matokeo mazuri dhidi yao.
"Hii ni siku ya kihistoria kwa mkoa wa Tabora, Kwa mashabiki wetu hii itakuwa zaidi ya sikukuu ya mpira wa miguu." alisema Kopunovic.
"Ninajiamini kwa kiasi kikubwa kama ambavyo wachezaji wangu wanajiamini Sihofii kama ambavyo wachezaji wangu hawana hofu Nategemea mashabiki kujaa na nina matumaini tuko vizuri."
Baada ya mchezo huu, Simba itaelekea mkoani Mwanza kujiandaa na mchezo mwingine wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC, utakaopigwa Februari 9 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.