TPLB KUSOGEZA MBELE MECHI ZA LIGI KUU MPAKA FEBRUARI
kiporo cha Simba na Azam kilichotarajiwa kupigwa Januari Mosi hakitapigwa tena sambamba na mechi nyingine za viporo kutokana na Bodi ya Ligi (TPLB) kuweka bayana kuwa ni ngumu kucheza kwa kubanwa na kalenda ya michuano tofauti ikiwamo fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023.
Michuano hiyo itapigwa kati ya Januari 13 hadi Februari 11, 2024 nchini Ivory Coast, na Tanzania ni miongoni mwa timu shiriki, hivyo kufanya baadhi ya mechi za Ligi Kuu kuvurugwa kwa sasa ikiwamo hiyo ya Simba na Azam na ile ya Januari 4 kati ya Simba dhidi ya Geita Gold, sambamba na kiporo cha Yanga na Dodoma Jiji.
Simba na Yanga kwa sasa zinacheza mechi za viporo, Simba ikianza dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Uhuru, KMC utachezwa Desemba 23, Mashujaa umepangwa kuchezwa Desemba 26 ugenini Uwanja wa Lake Tanganyika na Tabora United kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ni Desemba 29.
Hata hivyo, mechi na Tabora United nayo haina uhakika kama itachezwa kwani tayari mashindano ya Kombe la Mapinduzi yatakuwa yameanza na Simba inashiriki. Mashindano hayo yanaanza Desemba 28 Unguja, Zanzibar. Kwa upande wa Yanga, mechi ya Desemba 29 dhidi ya Mashujaa nayo iko kwenye hatihati kwani Kombe la Mapinduzi litakuwa limeanza.
Yanga baada ya mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, itakuwa na mechi nyingine dhidi ya Tabora United itakayochezwa Desemba 22 na ya Kagera Sugar itakuwa Desemba 26 - zote zikichezwa ugenini.
Kutokana na kuwepo kwa mwingiliano wa ratiba ya Ligi Kuu na Kombe la Mapinduzi, TPLB imesogeza mbele mechi zote za Januari na sasa zitachezwa baada ya michuano ya Afcon kumalizika Februari, mwakani na ligi rasmi ndiyo itaendelea.
Ofisa Habari wa TPLB, Karim Boimanda ili kufafanua juu ya ratiba na mechi hizo, na alisema: "Mechi hizo zote zitachezwa baada ya Afcon kwani haitakuwa rahisi kucheza wakati Kombe la Mapinduzi linaendelea na timu hizo zinashiriki mashindano hayo na baada ya hapo ni Afcon."
Hadi jana, Simba imecheza mechi tisa ikiwa nyuma mechi nne kwani timu zingine zimeshacheza michezo 13 wakati Yanga jana Jumamosi ilifikisha mechi 1l na imebakiwa viporo viwili mkononi.